News

DARAJA LA NKONKILANGI LAONDOA KERO YA MAFURIKO, LAKOMBOA WANANCHI KIUCHUMI

DARAJA LA NKONKILANGI LAONDOA KERO YA MAFURIKO, LAKOMBOA WANANCHI KIUCHUMI

Singida, 18 Februari, 2026

Kukamilika kwa Daraja la Nkonkilangi kumeondoa adha ya muda mrefu kwa wananchi waliokuwa wakishindwa kuvuka Mto Nkonkilangi wakati wa mvua kubwa kutokana na mafuriko.

Mhandisi Dastan Singano amesema daraja hilo sasa linawawezesha wananchi kupita mwaka mzima bila hofu ya kukatika kwa mawasiliano, hali inayochochea ukuaji wa uchumi wa Wilaya ya Iramba na Mkoa wa Singida kwa ujumla.

Hadi kukamilika kwake Oktoba 2025, mradi ulitoa ajira 272 kwa wazawa, wakiwemo wanawake 20 na wanaume 252.

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu, huku akitoa wito kwa wananchi kutunza daraja hilo ili lidumu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Nkonkilangi, Bi. Halima Amasi amesema daraja hilo limeondoa changamoto kwa wanafunzi na wananchi waliokuwa wakishindwa kuvuka mto wakati wa mvua.

Wananchi akiwemo Bw. Juma Mabula, Bi. Suzana Ramadhani na Bw. Ramadhani Mohamed wamesema sasa wanatumia dakika 10 hadi 15 kufika maeneo yao ya biashara na mashamba, tofauti na awali walipokuwa wakikumbwa na hatari ya kusombwa na maji.

Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Patrick Zulu, ameishukuru Serikali kwa kuwaamini wakandarasi wazawa na kusisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo pamoja na kutoa taarifa mapema endapo kutatokea changamoto yoyote.