TANROADS YAKAMILISHA DARAJA LA NKONKILANGI KUUNGANISHA SINGIDA NA SIMIYU
Singida, 18 Februari, 2026
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida umekamilisha ujenzi wa Daraja la Nkonkilangi linalounganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu, hatua itakayorahisisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano amesema daraja hilo limejengwa kupitia Mradi wa Dharura wa majanga yaliyotokana na mvua kubwa za El-Nino na kimbunga Hidaya vya mwaka 2023 na 2024, vilivyosababisha kukatika kwa mawasiliano baada ya baadhi ya madaraja kuharibika au kufunikwa na maji.
Amesema daraja hilo lina upana wa meta 11.25, likijumuisha meta 8.0 za njia ya magari mawili kwa wakati mmoja na njia za watembea kwa miguu zenye upana wa meta 1.625 kila upande. Aidha, mradi umehusisha ujenzi wa barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilometa 1.0 pamoja na makalavati 10.
Daraja hilo limejengwa kwa zege imara lenye uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 100 na kuruhusu magari yenye uzito wa hadi tani 50 kupita kwa usalama.
Mradi huo umegharimu Shilingi bilioni 6.6, fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Dharura (CERC), na kutekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya M/s J.P Traders Limited chini ya usimamizi wa Kitengo cha Uhandisi cha TANROADS (TECU).
Daraja la Nkonkilangi ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Singida na Simiyu kupitia barabara za Shelui – Sekenke – Tulya – Tyegelo, Tyegelo – Chemchem na Chemchem – Nyahaa – Sibiti hadi Meatu mkoani Simiyu. Pia linaunganisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Kitangili na vijiji vya Wilaya ya Iramba na Meatu.