News

DC DODOMA ARIDHISHWA NA MAENDELEO UJENZI KIWANJA CHA  NDEGE MSALATO NA BARABARA YA MZUNGUKO

DC DODOMA ARIDHISHWA NA MAENDELEO UJENZI KIWANJA CHA  NDEGE MSALATO NA BARABARA YA MZUNGUKO

Dodoma, 18 Februari, 2026

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe.Jabir Shekimweri, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, wametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Outer Ring Roads) jijini Dodoma, kwa ujumla wameridhishwa na utekelezaji.

Akizungumza leo tarehe 18 Februari 2026 baada ya kukagua miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya amesema kasi na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ujenzi huo ni kubwa, na aimepongeza Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) kwa kasi na hatua kubwa ya utelekezaji akieleza kuwa miradi hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi na kuboresha miundombinu ya usafiri Makao Makuu ya nchi nchi, ambayo ni Dodoma.

“Nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato pamoja na barabara ya mzunguko wa nje, hii ni miradi mikubwa na ya kimkakati kwa maendeleo ya Dodoma na Taifa kwa ujumla,” amesema Mhe. Shekimweri. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Miradi ya Maendeleo mkoa wa Dodoma (TANROADS), Mhandisi Colman Ramadhani amesema miundombinu ya kiwanja hadi sasa imefikia asilimia 83 na upande wa majengo sasa ni asilimia 67.

Pia amesema TANROADS itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati uliopangwa.

Nayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango na ubora unaokubalika na kuleta tija kwa wananchi.