DARAJA LA JANGWANI KUBADILISHA MANDHARI YA DAR KWA KUPANDA MITA 8 JUU YA USAWA WA SASA
Dar es Salaam, 17 Februari, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Jangwani, mradi mkubwa wa kimkakati utakaobadilisha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuinuka takribani mita 8 juu ya usawa wa barabara iliyopo sasa, hatua inayolenga kudhibiti changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara yanayosababishwa na maji kutoka Mto Msimbazi.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Mradi, Mhandisi Leonard Ngayungi, amesema daraja hilo ni sehemu ya Programu ya Maendeleo ya Bonde la Msimbazi inayotekelezwa kupitia vipengele vitano, mojawapo ikiwa ni ujenzi wa miundombinu imara ya kuhimili mafuriko.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ngayungi, urefu wa eneo lote la mradi ni kilometa 1.2, ambapo daraja lenyewe lina urefu wa mita 390 na upana wa mita 41, huku sehemu inayobaki ikiwa ni barabara za maingilio. Mradi huo pia unahusisha miundombinu ya waenda kwa miguu na njia za waendesha baiskeli pamoja na ujenzi wa kituo cha mabasi ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT), kitakachohudumia abiria wa viwanja vya michezo vitakavyojengwa katika eneo hilo kupitia taasisi nyingine ndani ya programu hiyo.
Ameeleza kuwa mkandarasi alianza kwa kuhamisha miundombinu ya umeme, maji na mawasiliano, sambamba na ujenzi wa barabara ya mchepuko ili kuhakikisha magari yanaendelea kupita wakati ujenzi ukiendelea.
Kwa sasa, kazi kubwa inayoendelea ni ujenzi wa misingi ya daraja (piles na pile caps), nguzo kuu (piers) na maandalizi ya eneo la juu la kupitisha watumiaji (deck). Daraja hili litakuwa na jumla ya nguzo za msingi takribani 496 zenye urefu wa mita 35 hadi 42 chini ya ardhi kulingana na tathmini ya udongo; hadi sasa nguzo 404 tayari zimekamilika.
“Kukamilika kwa nguzo za msingi kutafuatiwa na ujenzi wa vitako vya nguzo (pile caps), kisha nguzo kuu (piers), na baadaye eneo la juu lenye beams na deck litakalounganishwa na barabara za maingilio tayari kwa kupitisha magari na watumiaji wengine,” amefafanua kitaalamu Mhandisi Ngayungi.
Mbali na kudhibiti mafuriko, eneo la Jangwani linatarajiwa kuwa kitovu kipya cha kijamii na kiuchumi, likijumuisha viwanja vya michezo, maeneo ya burudani pamoja na maendeleo ya kibiashara na makazi, hatua itakayorejesha hadhi ya eneo hilo kama sehemu muhimu ya mikusanyiko na shughuli za kijamii kama ilivyokuwa hapo awali.
Mhandisi Ngayungi ameishukuru Serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa daraja hilo litamaliza adha ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara wakati wa masika, kulinda maisha na mali za wananchi, na kutoa njia salama na rafiki kwa waenda kwa miguu na waendesha baiskeli.
“Awali eneo hili lilikuwa hatarishi kwa watumiaji wa barabara kutokana na mafuriko yaliyokuwa yakikatiza mawasiliano kwa saa kadhaa na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na kuhatarisha maisha. Mradi huu ni suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo,” amesisitiza.