News

UHIFADHI WA MNARA WA ASKARI WAIMARISHA UTAMBULISHO WA JIJI NA KUONGEZA FAHARI YA WAKAZI WA DAR ES SALAAM

UHIFADHI WA MNARA WA ASKARI WAIMARISHA UTAMBULISHO WA JIJI NA KUONGEZA FAHARI YA WAKAZI WA DAR ES SALAAM

Dar es Salaam, 16 Februari, 2026

Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuweka mandhari mazuri na mchoro uliobakiza alama muhimu ya kihistoria ya Mnara wa Askari wakati wa utekelezaji wa mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT–Mwendokasi).

Awali, wakati ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi huo unaoanzia katikati ya jiji kuelekea Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere ulipoanza, wakazi wengi walionesha hofu kuwa mnara huo ungeondolewa kupisha ujenzi.

Mnara huo uliopo katikati ya barabara umeendelea kuwa kielelezo cha heshima kwa mashujaa waliopigana vita pamoja na alama mahsusi ya Jiji la Dar es Salaam kwa wenyeji na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Bw. Maganga Shiwembo, mkazi wa Kigamboni anayejishughulisha na uendeshaji wa bodaboda katika kituo cha Mnara wa Askari Posta, amesema kuwa walipoona shughuli za upimaji zikianza walihofia kuondolewa kwa mnara huo na hivyo kuwasilisha maombi yao kwa wakandarasi wasiondoe alama hiyo ya kihistoria.

Huu Mnara wa Askari ni alama na kielelezo tosha. Wapo watalii kutoka nje ya nchi wanaokuja kupata historia, na wapo wananchi kutoka mikoani wanaokuja kupiga picha kuonesha wamefika Dar es Salaam.

 "Tuliingiwa na hofu sana tulipoona maandalizi ya ujenzi, lakini tunaishukuru sana Serikali kwa kuubakiza mnara huu na kuuongezea ubora wa mandhari yake. Sasa unaonekana vizuri zaidi na tunaomba uendelee kuwepo kizazi hadi kizazi," amesema Bw. Maganga.

Ameongeza kuwa mradi wa mabasi yaendayo haraka umekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa jiji kwa kurahisisha usafiri, kupunguza muda wa safari na kupunguza foleni zilizokuwa kero kwa miaka mingi.

Mbali na kuboresha usafiri, Bw. Maganga amesema mradi huo pia umependezesha jiji kutokana na michoro na mpangilio mpya wa barabara, hali ambayo kwa baadhi ya watu waliokaa muda mrefu bila kufika jijini, imewafanya kupotea njia kutokana na mabadiliko makubwa ya miundombinu.

Kama hapa kwenye Mnara wa Askari, unakuta mtu anataka kwenda Tegeta lakini anajikuta kapotea kwa sababu zamani mabasi yalikuwa yanapandia Posta ya zamani. Sasa mazingira yamebadilika sana. Wanapouliza, tunawasaidia kuwaelekeza na tumeelekeza watu wengi sana, amesema Bw. Maganga.

Hatua ya TANROADS kubakiza na kuboresha mandhari ya Mnara wa Askari inaonesha namna ambavyo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati unaweza kwenda sambamba na utunzaji wa urithi wa kihistoria, kuimarisha utambulisho wa jiji na kuongeza fahari ya wananchi.