News

ZAIDI YA BIL. 600 ZAWEKEZWA KUJENGA MIUNDOMBINU YA MABASI YA MWENDOKASI DAR ES SALAAM; AWAMU YA KWANZA NA MBILI ZATOA HUDUMA

ZAIDI YA BIL. 600 ZAWEKEZWA KUJENGA MIUNDOMBINU YA MABASI YA MWENDOKASI DAR ES SALAAM; AWAMU YA KWANZA NA MBILI ZATOA HUDUMA

Dar es Salaam, 15 Februari, 2026

Zaidi ya shilingi Bilioni 600 zimewekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam, mradi unaotekelezwa kwa awamu sita kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri kwa wakazi na wageni wa jiji hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Ujenzi wa Mradi wa BRT kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Frank Mbilinyi, amesema hadi sasa awamu mbili zimekamilika na zinaendelea kutumika, huku awamu ya tatu ikiwa imefikia asilimia 98 ya utekelezaji.

Ameeleza kuwa awamu ya kwanza iliyoanza kujengwa mwaka 2015 inahusisha barabara kutoka katikati ya jiji hadi Kimara, ambayo imekamilika na imekuwa ikitumika tangu mwaka 2025.  Awamu ya pili ni barabara ya Kilwa hadi Mbagala, nayo imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa awamu ya tatu, amesema inahusisha ujenzi kutoka katikati ya jiji kupitia barabara ya Nyerere hadi Gongolamboto, ambapo ujenzi umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu kabla ya kukabidhiwa rasmi Serikalini.

Mhandisi Mbilinyi amefafanua kuwa awamu ya nne inaanzia katikati ya jiji kuelekea Tegeta kupitia barabara ya Ally Hassan Mwinyi, na itahusisha pia kipande cha Mwenge hadi Ubungo kitakachounganisha na njia ya Morogoro. Utekelezaji wa awamu hii umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026.

Aidha, awamu ya tano itahusisha ujenzi kuanzia barabara ya Mandela (Ubungo) kuelekea Bandarini, pamoja na barabara ya Tabata kuanzia Segerea, kukatiza Mandela hadi Kigogo. Kwa sasa, maandalizi yanaendelea ikiwemo mchakato wa kumpata mkandarasi.

Awamu ya sita ipo katika hatua ya mpango na itahusisha barabara ya Moi Kibaki pamoja na kuendeleza miundombinu iliyopo, ikiwemo kupanua kutoka Kimara hadi Mbezi, na kuongeza mtandao wa awamu ya pili kutoka Mbagala Rangitatu hadi Vikindu.Amesema awamu ya kwanza hadi ya tatu zinafadhiliwa na Benki ya Dunia, huku awamu ya nne hadi ya sita zikifadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).