News

KONGOWE KUJENGWA DARAJA LA JUU; MSURURU WA FOLENI WAANZA KUWA HISTORIA

KONGOWE KUJENGWA DARAJA LA JUU; MSURURU WA FOLENI WAANZA KUWA HISTORIA

Dar es Salaam,  12 Februari, 2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati jijini Dar es Salaam yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha mtiririko wa usafiri katika maeneo yenye changamoto kubwa za foleni.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema ujenzi wa daraja la juu (flyover) eneo la Kongowe pamoja na barabara unganishi ya Mbagala Rangi Tatu – Kongowe (Km 3.8) unaendelea vizuri tangu ulipoanza Agosti 2025.

Ameeleza kuwa daraja hilo litawezesha magari kupita kwa njia tofauti bila kukatizana, hivyo kuondoa hitaji la taa za kuongozea magari katika eneo hilo.

Magari yanayotoka Kibada kuelekea Kongowe yatapita chini ya daraja na kuungana na njia ya kuelekea Mbagala Rangi Tatu, huku yale yanayotoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Mkuranga, Mtwara na Lindi yakipita juu ya daraja hilo. Barabara hiyo itakuwa na njia nne (four lanes) ili kuongeza uwezo wa kupitisha magari kwa wakati mmoja.

“Kwenye mfumo huu hakutakuwa na magari kupishana au kusubiri taa; kila gari litapita katika mkondo wake maalum, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa msongamano,” amesema Mhandisi Kyamba.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kutoka China chini ya usimamizi wa wataalamu wa TANROADS.Aidha, Mhandisi Kyamba ametaja miradi mingine ya kimkakati inayoendelea jijini humo kuwa ni ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (Km 41), unaotekelezwa na kampuni ya Estim kwa gharama ya shilingi bilioni 83.

Hadi sasa, Km 8 zimejengwa kwa kiwango cha lami na kuwekwa alama muhimu za barabarani, na magari tayari yanapita.Mradi mwingine ni wa Kimara–Bonyokwa unaotekelezwa na kampuni ya Nyanza.Kwa upande wake, mkazi wa eneo la Tuangoma–Kongowe, Bw. Tamimu Seif, amesema Kongowe ni kiunganishi muhimu cha barabara kutoka Tuangoma, Mbagala Rangi Tatu, Mkuranga hadi Mlemlemu, hivyo ujenzi wa daraja hilo utakuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya foleni na ajali zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.