SERIKALI YALETA MATUMAINI MAPYA MTONGANI, MKWAJUNI NA KIGAMBONI YAJENGA MADARAJA MAKUBWA MATANO
Dar es Salaam, 11 Februari, 202
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetekeleza ujenzi wa madaraja makubwa matano katika maeneo ya Mtongani–Kunduchi, Mkwajuni na Kigamboni, hatua inayotoa suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto ya mafuriko iliyokuwa ikiathiri wakazi wa maeneo hayo kufuatia mvua kubwa za El-Nino za mwaka 2023/2024.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema miundombinu hiyo mipya imejengwa kwa viwango vya kisasa ili kuhimili maji mengi na kuhakikisha mawasiliano hayakatiki tena wakati wa masika.
Alieleza kuwa madaraja hayo ni:Daraja la Mtongani (urefu mita 20) pamoja na barabara za maungio zenye urefu wa Km 1.2 – linajengwa na kampuni ya Shandom (China);Daraja la Mkwajuni (mita 20) – mkandarasi ni Kings Builders (mzawa);Daraja la Kigogo (mita 50, kina mita 10) pamoja na barabara za maungio mita 680 kutoka Ilala Boma hadi mzunguko wa Kigogo;Daraja la Kisarawe II na Amani Gomvu (Wilaya ya Kigamboni) – yanajengwa na kampuni ya Osaka (mzawa);Daraja la Nguva (mita 60) lenye njia za maingilio mita 300 – linajengwa na kampuni ya Nyanza Ltd (mzawa).
“Madaraja yote yapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, ikiwemo uwekaji wa lami kwenye barabara za maungio na alama muhimu za barabarani. Baadhi ya miradi imefikia asilimia 85 hadi 90 ya utekelezaji, na ifikapo Machi 2026 itakuwa imekamilika rasmi,” amesema Mhandisi Kyamba.
Ameongeza kuwa miradi hiyo inaenda sambamba na usimikaji wa jumla ya taa 206 za barabarani ili kuongeza usalama kwa watumiaji hususan nyakati za usiku.Mhandisi Kyamba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi bilioni 71 kupitia miradi ya dharura (CERC), fedha ambazo zimewezesha utekelezaji wa miundombinu hiyo kwa wakati.
Amesisitiza kuwa madaraja hayo yamejengwa kwa ubora wa hali ya juu chini ya usimamizi wa Kitengo cha Usanifu cha TANROADS (TECU) na yamezingatia uwezo wa kupitisha maji mengi ili kuondoa hatari ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua kubwa.