KING’ORI YAWA MASHUHUDA WA MAFANIKIO YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA, TAA 136, MADARAJA SITA NA BIASHARA ZA USIKU ZASHIKA KASI KING’ORI
Arusha
11/02/2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema utekelezaji wa miradi ya miundombinu chini ya Serikali ya Awamu ya Sita umeleta mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi katika eneo la King’ori wilayani Arumeru mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya Siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Februari 08, 2026 wakati wa tathmini ya Siku 100 za Rais Samia katika sekta ya ujenzi, Mhe. Ulega amesema Serikali imetekeleza na kukamilisha mradi muhimu wa barabara a King'ori pamoja na kuweka taa za barabarani na miundombinu ya usalama ndani ya siku 100, hatua iliyobadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi wa King’ori.
Amesema jumla ya taa za barabarani 136 zimefungwa na kusambazwa katika eneo lote la King’ori, hatua iliyoongeza usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi, hususan biashara za nyakati za usiku.
Aidha, madaraja sita (6) yamejengwa ili kuruhusu maji kupita kwa usalama, pamoja na ujenzi wa kilometa 1.08 ya barabara ya lami.
“Tunayo historia ya mafuriko yaliyokuwa yakisababisha wananchi kusombwa na maji na kupoteza maisha. Kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, mradi huu umejengwa na kukamilika ndani ya Siku 100 za Rais Samia, na wananchi wa King’ori wana ushahidi wa moja kwa moja wa mafanikio haya,” amesema Mhe. Ulega.
Katika kuimarisha ustawi wa wananchi, Waziri Ulega amesema Serikali pia imejenga vituo maalumu vya wananchi kupumzikia na kujikinga na jua pamoja na mvua, kama sehemu ya kuzingatia mahitaji ya kijamii sambamba na ujenzi wa barabara.
Akizungumzia mchango wa wataalamu wa ndani, Mhe. Ulega amempongeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, kwa ubunifu na uamuzi wa kuongeza idadi ya taa zaidi ya ilivyokuwa kwenye mpango wa awali.
“Hizi taa huenda hazikuwa zote kwenye mpango wa mwanzo, lakini kutokana na maelekezo ya Rais Samia kwamba kila barabara inayojengwa iwekwe taa, Mhandisi Massawe aliweka zaidi ya taa 80. Baadaye kulikuwa na ombi la taa zaidi ya 50, na leo tunayo jumla ya taa 136 katika King’ori,” amesema.
Mhe. Ulega ameongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha barabara yote kuanzia Arusha hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) inawekewa taa, akibainisha kuwa ni barabara ya kimkakati kwa utalii na uchumi, na pia ni lango muhimu la kuingia nchini.
Kwa nyakati tofauti Wananchi wa King’ori wameeleza kuridhishwa na matokeo ya miradi hiyo.
Afisa usafirishaji maarufu kama bodaboda, Richard Kaaya amesema kuwa awali walishindwa kufanya kazi nyakati za usiku kutokana na giza na ukosefu wa usalama, hali ambayo sasa imebadilika.
“Kwa sasa tunafanya kazi hadi usiku bila hofu, kuna usalama mkubwa kutokana na taa hizi,” amesema Juma.
Naye mkazi wa eneo hilo, Hillary Mollel amesema maendeleo yaliyoletwa na Serikali yamebadilisha taswira ya eneo la Malula, ambalo awali lilikuwa likidharaulika.
“Zamani Malula ilionekana kama eneo la watu wa hali ya chini, lakini sasa kila mtu anatafuta kuishi hapa kutokana na maendeleo makubwa yaliyoletwa na uongozi wa Rais Samia,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega, kazi iliyofanyika King’ori ni mfano wa juhudi zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini, zikilenga kuboresha miundombinu, kuongeza usalama na kukuza uchumi wa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi yenye tija kwa jamii.