News

MADARAJA SABA YALIYOJENGWA MOROGORO YATOA AJIRA KUBWA KWA WAZAWA

MADARAJA SABA YALIYOJENGWA MOROGORO YATOA AJIRA KUBWA KWA WAZAWA

Morogoro, 08 Februari, 2026

Wakazi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na mikoa ya jirani wamenufaika kwa kiasi kikubwa na ujenzi wa madaraja saba yaliyotekelezwa kupitia miradi sita ya dharura (CERC), kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, baada ya miundombinu hiyo kuharibiwa na mvua kubwa za El Niño na Kipunga Hidaya zilizonyesha mwaka 2023/2024.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika, amesema mvua hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa madaraja yaliyopo kwenye barabara za mikoa na barabara kuu, hali iliyosababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara kutokana na kukatika kwa mawasiliano kwa saa na hata siku kadhaa.

Mhandisi Rambika ameyataja madaraja hayo kuwa ni Mjonga (mita 80), Bwage (mita 25), Doma (mita 20), Chakwale (mita 80), Nguyami (mita 100), Ngerengere (mita 30.6) na Kihonda (mita 30).

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo sita yenye madaraja saba umefanikisha upatikanaji wa ajira 1,085, ambazo zilitolewa na wakandarasi wazawa waliotekeleza ujenzi wa madaraja hayo.

Aidha, wananchi mbalimbali wamenufaika kiuchumi kwa kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za malazi, usafiri wa bodaboda na mabasi, uuzaji wa chakula, vinywaji, matunda pamoja na bidhaa nyingine.

Dereva wa Kampuni ya Facebook Safari, Bw. Salehe, anayefanya safari za Handeni – Dumila – Gairo, amesema awali baada ya kukatika kwa daraja walilazimika kusitisha huduma za usafiri, lakini baada ya kukamilika kwa ujenzi, safari sasa huchukua saa moja na nusu hadi mbili, tofauti na awali ambapo walitumia zaidi ya saa tatu.

Kwa upande wake, Afisa Usafirishaji na mwendesha bodaboda, Bw. Haji Shabaan, amesema walishindwa kutoa huduma ya usafiri wa bodaboda kipindi cha mvua kutokana na maji kupita juu ya daraja kwa kasi kubwa.

Amesema ujenzi wa daraja jipya umeondoa changamoto hiyo kwani maji hayatapita tena juu ya daraja. Naye Bw. Kelvin Ndedya, mwajiriwa wa Kampuni ya Halem Construction Co. Ltd na mwendeshaji wa mashine ya kushindilia barabara, amesema mradi huo umetoa ajira kwa vijana wengi wazawa, hali iliyosaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa.