News

TANROADS MKOA WA MOROGORO YAJIVUNIA KUTEKELEZA UJENZI WA MADARAJA SABA YALIYOHARIBIWA NA EL-NINO NA KIMBUNGA HIDAYA * WATUMIAJI WAASWA KUITUNZA MIUNDOMBINU

TANROADS MKOA WA MOROGORO YAJIVUNIA KUTEKELEZA UJENZI WA MADARAJA SABA YALIYOHARIBIWA NA EL-NINO NA KIMBUNGA HIDAYA

* WATUMIAJI WAASWA KUITUNZA MIUNDOMBINU

Morogoro, 08 Februari, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro imejivunia kutekeleza ujenzi wa madaraja saba yaliyoharibiwa na mvua kubwa za el-nino na kimbuga Hidaya vilivyotokea mwaka 2023/24.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika amesema mkoa huo wenye mtandao wa barabara Km. 2071.23 ulipata changamoto katika baadhi ya madaraja yaliyopo katika barabara kuu na za mkoa za Morogoro-Dodoma; Iyogwe-Chakwale-Giloli; Mvomero-Ndole-Kibati-Lusanga; Morogoro-Iringa (TANZAM Highway); na Turiani-Magole, yaliathirika kwa kukatika, na mengine kusombwa na maji mengi ya mafuriko na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara hizo.

Mhandisi Rambika amesema serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ilitoa kiasi cha shilingi Bil. 37 za mfuko wa dharura wa Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miradi sita yenye madaraja saba mapya na barabara unganishi.

Ameyataja madaraja hayo kuwa ni Chakwale lenye urefu wa mita 80; Nguyami mita 100; Mjonga (80m); Bwage (25m); Doma (20m); Kihonda (30m) na Ngerengere (30.6m).

Mhandisi Rambika amesema kukamilika kwa madaraja hayo kutaleta manufaa makubwa kwa watumiaji wa barabara hizo na kukuza biashara, uchumi na pato la taifa kwa kuwa kutakuwa na usafiri wa uhakika kutoka upande mmoja na kwenda mwingine, tofauti na awali.

“Miundombinu imeimarika maana haya madaraja yaliathirika na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wake ikiwemo kusombwa kwa mali,” amesema Mhandisi Rambika.

Amesema madaraja yote yamejengwa na makampuni sita ya wazawa kwa kiwango cha juu na kunyanyuliwa kwa tuta la barabara, ambalo halitaruhusu maji kujaa kipindi chochote cha mvua. Makampuni hayo ni ASABHI, Halem, Osaka, COBEX, Jambela na Nyota.

Halikadhalika, Mhandisi Rambika amesema madaraja hayo yatasimikwa taa kwa ajili ya usalama wa mbiundombinu hii na watumiaji kwa nyakati za usiku, ambapo ametoa rai kwa wakazi kuitunza miundombinu.

Mhandisi Rambika ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuridhia maombi na kuidhinisha kiasi cha fedha kilichokamilisha ujenzi wa madaraja hayo katika mradi wa dharura.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ASABHI ya wazawa inayojenga daraja la Chakwale, Ibrahim Nyambacha ameishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi ambayo wameifanya kwa uaminifu na umahiri, na kuomba waendelee kuaminika kwa kupewa kazi nyingine.

Mtendaji wa Kijiji cha Chakwale, Bw. Nickson Diausa amesema kutokana na adha waliyokuwa wakipata shida kwa ajili ya kupita maeneo haya, na ameahidi watahakikisha miundombinu hii inalindwa ili isiweze kuhujumiwa ili iweze kudumu kwa miaka iliyokusudiwa.

Naye Mhandisi wa Madaraja wa ASABHI, Justine Magita amesema daraja hili litakuwa msaada mkubwa kwa watumiaji wake maana linapita magari makubwa ya abiria na mizigo, bodaboda na waenda kwa miguu.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Matomondo, Bw. Shaaban Hussein, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya ASABHI katika ujenzi wa daraja la Bwage, amesema awali daraja lililokuwepo lilisababisha maafa kwa wamama wajawazito na watoto waliosombwa na maji mengi yaliyokuwa yakitoka Kiteto na Dodoma, ila kwa sasa wanaamini hali itakuwa nzuri, na ameishukuru serikali kwa kazi kubwa ya kujengwa kwa daraja hili.

Naye Mkazi wa Bwage, Bw. Salum Wakili amesema ujenzi wa daraja hili umekuwa suluhisho la kudumu kwa kuwaondolea mafuriko na sasa wanawake wanajawazito, watoto, Wazee na wagonjwa wengine wanaokwenda kupata matibabu kwenye hospital ya Bwagala, watapita juu ya daraja bila adha yeyote.s

Kwa upande wake, Bw. Ramadhani Tundunguro anasema wamepata adha kubwa ya kuvushwa kwa kubebwa mabegani na kutozwa bei kubwa wakati wa kuvushwa wao na mizigo yao, lakini sasa anashukuru kutokana na daraja kuwa juu na haliwezi kupitisha maji kwa juu.