News

SIKU 100 ZA RAIS SAMIA, TAA ZA BARABARANI ZAIMARISHA USALAMA NA UCHUMI MBEYA

SIKU 100 ZA RAIS SAMIA, TAA ZA BARABARANI ZAIMARISHA USALAMA NA UCHUMI MBEYA

Mbeya.

04/02/2026

Ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya imefanikiwa kutekeleza miradi ya dharura (CERC) pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika madaraja makuu matatu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema utekelezaji wa miradi hiyo ulitokana na miongozo ya Serikali iliyotolewa kwa nyakati tofauti, ikiwemo maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, pamoja na maelekezo ya kiutendaji kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour, waliotaka kufanyika kwa tathmini ya kina ya hali ya miundombinu ya barabara na kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kuboresha usalama mkoani Mbeya.

Amesema katika barabara ya TANZAM, eneo la daraja la Sungwa, TANROADS iliagizwa kuweka taa za barabarani, ambapo hadi sasa jumla ya taa 40 zimekamilika kufungwa.

Aidha, amesema katika barabara ya Makongorosi kuelekea mipakani mwa mikoa ya Singida na Tabora, TANROADS imeweka taa za barabarani katika madaraja mawili makubwa ya Lupa na Bitimanyanga, ambapo zaidi ya taa 39 zimewekwa katika daraja la Lupa na zaidi ya taa 42 katika daraja la Bitimanyanga.

Ikumbukwe kuwa utekelezaji wa maagizo hayo umefanikiwa kutokana na usimamizi wa karibu, ufuatiliaji wa mara kwa mara na maamuzi ya haraka ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, ambaye ameendelea kutoa mwelekeo thabiti katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vya juu vya ufanisi, weredi na uwajibikaji.

Kwa upande wao, wananchi wa maeneo husika wamesema uwepo wa taa za barabarani umeleta mabadiliko chanya katika maisha yao ya kila siku, hususan katika kuimarika kwa usalama na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.

Mkazi wa Lupa Tingatinga, Ailice John Mpangala, amesema kuwa kabla ya kuwekwa kwa taa, wananchi walikuwa na hofu ya kutumia barabara nyakati za usiku kutokana na giza na hatari za ajali.

Naye Bahati Mwampetele, mkazi wa Lupa Tingatinga, amesema uwepo wa taa za barabarani umewezesha wananchi kufanya shughuli zao za kibiashara hadi nyakati za usiku, tofauti na ilivyokuwa awali.

“Zamani tulikuwa tunalala mapema, lakini sasa kutokana na uwepo wa taa tunaweza kufanya biashara hadi usiku na kipato kimeongezeka,” amesema.

Kwa upande wake, Martine William, mkazi wa Kata ya Lupa, amesema uwekaji wa taa umeimarisha usalama na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

“Taa zimeleta mwanga na usalama. Wajasiriamali wengi sasa wanafanya kazi zao bila hofu, hali ambayo haikuwepo hapo awali,” amesema.

Mhandisi Bishanga ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ndani ya siku 100 za Rais Samia umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza hatari za ajali, kuondoa hofu kwa wasafiri na kuwezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa muda mrefu zaidi.