News

WANANCHI WA MKOA WA LINDI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA MADARAJA MAKUBWA MATANO YAKIWEMO SOMANGA MTAMA NA MBWEMKURU

WANANCHI WA MKOA WA LINDI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA MADARAJA MAKUBWA MATANO YAKIWEMO SOMANGA MTAMA NA MBWEMKURU

Lindi, 01 Februari, 2026

Wakazi wa wilaya na vitongoji mbalimbali vya Mkoa wa Lindi wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kurejesha mawasiliano kati ya mikoa ya Lindi na Pwani (Kilwa), kufuatia utekelezaji wa miradi ya dharura ya ujenzi wa barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua kubwa za El Niño na Kimbunga Hidaya cha mwaka 2023/24.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Dotto John Chacha, amesema miradi hiyo imefikia hatua za mwisho za ukamilishaji, hali itakayowezesha upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika katika majira yote ya mwaka.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo, Mhandisi Chacha amesema TANROADS inatekeleza jumla ya miradi 13 ya dharura mkoani humo, ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa matano katika barabara kuu ya Lindi–Dar es Salaam.

Madaraja hayo ni Daraja la Somanga Mtama lenye urefu wa mita 60, Kipweta (mita 40), Njenga (mita 60), Mikereng’ende (mita 40) pamoja na Daraja la Mbwemkuru 1.

Ameongeza kwa kusema kuwa, pamoja na ujenzi wa madaraja hayo, TANROADS imenyoosha na kuinua matuta ya barabara na kujenga boksi kalavati tano zenye midomo mikubwa karibu na maeneo ya madaraja, hatua inayolenga kuboresha upitishaji wa maji mengi na kuondoa tatizo la mafuriko yaliyokuwa yakikata mawasiliano mara kwa mara.

“Mkoa wa Lindi una mtandao wa barabara kuu na za mkoa zenye jumla ya urefu wa kilomita 1,320. Mwaka 2023/24, mvua kubwa za El Niño na Kimbunga Hidaya zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja, hali iliyopelekea kukatika kwa mawasiliano katika barabara za Marendego–Mingoyo, Nangurukuru–Liwale, Liwale–Nachingwea na Kiranjeranje–Namichiga,” amesema Mhandisi Chacha.

Akifafanua zaidi amesema, maeneo yote yaliyoathiriwa tayari yamejengwa upya kwa kuwekwa miundombinu imara na rafiki kwa mazingira, itakayowezesha maji kupita kwa urahisi na kuzuia kujirudia kwa mafuriko.

Amesema miradi hiyo ya madaraja na makalavati inakwenda sambamba na usimikaji wa taa za barabarani zenye kutumia mfumo wa umeme wa jua (Solar), ili kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu hiyo pamoja na watumiaji wa barabara hiyo, na pia kufanikisha shughuli za kijamii ikiwemo biashara ndogondogo zitakazowaongezea wananchi kipato na kukuza uchumia wao.

Mhandisi Chacha amesema miradi hiyo imetoa ajira takribani 300 za vijana kupitia wakandarasi wa nje na Wazawa ambao ni China Kampuni ya Makapo Constractors, Harem, ME Contructor na Jambela.

Mhandisi Chacha ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kiasi cha Shilingi Bil. 119 kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo, ambayo sasa imewapa kicheko na furaha wakazi na watumiaji wa barabara Kuu hiyo, maana sasa wanauhakika wa safari katika majira yote ya masika na kiangazi.

“Ninamshukuru pia Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telac, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta, na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wa kufanya kazi usiku na mchana katika kufanikisha ujenzi wa hii miradi ya dharura inajengwa kwa kutumia viwango na kukamilika kwa wakati,” amesema Mhandisi Chacha. 

Kwa upande wake mkazi wa Somanga Mtama, Mzee Shaweji Kimbembe ameipa kongole serikali kwa kurudisha tabasamu kwa watumiaji wa barabara hiyo kuu, ambapo sasa wanauhakika mkubwa wa safari za kutoka Lindi kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ukiwemo Dar es Salaam, ambapo awali wakati wa mvua walikuwa wakitumia mitumbwi, kamba na kushikana mikono ili waweze kuvuka upande mmoja na kwenda mwingine kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali.

“Ninafurahi sana nimesimama juu kabisa ya hili daraja na hii barabara inamaana sasa hakuna maji ya mafuriko yatapita hapa tena, wananchi tulishughudia ujenzi wa kiwango uliofanyika kwenye ujenzi ikiwemo kuwekwa nondo na saruji kwa ujenzi wa nguzo zilizozamishwa chini na tunashukuru kwa kuwekwa taa kwani zitazalisha ajira kwa watu kufanya biashara ndogondogo, na hata sasa tunauhakika wa kusafirisha mazao yetu sehemu mbalimbali, hivyo tunamshukuru sana Rais na kutolea maamuzi ya ujenzi huu,” amesema Mzee Kimbembe.

Naye mkazi, Bw. Hamza Ahmed wa Mbwemkuru ameshukuru serikali kwa ujenzi wa daraja la Mbwemkuru 1, ambalo lilianza kuharibika mwaka 2000 kwa kumomonyoka kwa udongo kwenye makalavati na baadaye likakatika, lakini sasa wataalam wamewezesha ujenzi kwa kuongeza njia za kupita maji mengi na ujenzi wa makalavati matatu na kupandisha barabara. 

Amesema wakati wa mvua walipata adha kubwa ya kukatika kwa mawasiliano kati ya Lindi na Kilwa, kutokana na maji mengi kupita juu ya daraja la awali.

Kwa upande wake Bw. Mohamed Wadayi mkazi wa Wilaya ya Tunduru amesema miradi hii ya miundombinu imetoa ajira kwa vijana kutoka mikoa mbalimbali, ambapo ameiomba serikali kuendelea kutoa ajira za muda mrefu na mfupi katika miradi ya ujenzi ili vijana wengi waliopo nyumbani bila kazi kuweza kulitumikia taifa kwa ujenzi wa miundombinu.

Kwa nyakati tofauti Bi. Sikuzani Said, mamalishe na Bi. Tatu Hassan, mfanyabiashara wa samaki za kukaanga kwa pamoja wameishukuru serikali kwa kuwafungia taa kwenye maeneo ya Somanga Centre ambapo sasa zinawasaidia katika biashara zao hizo wanazofanya nyakati za usiku, na pia  zimepunguza uhalifu na ajali za mara kwa mara.