TANROADS YATOA ELIMU YA UELEWA WA PAMOJA KWA WANANCHI KUHUSU MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA KIBANJA–MBAMBO, MBEYA
Mbeya, 31 January 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara nchini kupitia utoaji wa elimu ya uelewa wa pamoja kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara.
Katika hatua hiyo,Wakala imetoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Katumba–Mbambo–Tukuyu, sehemu ya nne inayounganisha Kibanja hadi Mbambo mkoani Mbeya,ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu ya kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa ufanisi na kwa ushirikishwaji wa wananchi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msimamizi wa Hifadhi ya Barabara wa TANROADS Mkoa wa Mbeya,Bw. Christopher Chalange,amesema kuwa lengo la utoaji wa elimu hiyo ni kuwawezesha wananchi kuelewa kwa kina mradi unaotekelezwa pamoja na wajibu wao katika matumizi bora ya hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria, ili kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mradi kwa ufanisi na uwazi.
Bw. Chalange amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009, hifadhi ya barabara imeainishwa kuwa na upana wa mita 30 kila upande,hivyo kufanya upana wa jumla wa eneo la barabara kuwa mita 60. Ameeleza kuwa,kwa kuzingatia usanifu wa kitaalamu wa mradi huu,barabara itakayojengwa itatumia eneo la mita 22.5 kila upande bila kuathiri matakwa ya kisheria ya hifadhi ya barabara.
Ameongeza kuwa mkandarasi wa mradi tayari yupo uwandani na ameanza utekelezaji wa kazi za awali za ujenzi,huku akisisitiza umuhimu wa kuwafikia wananchi wanaonufaika na mradi huo kwa kuwapatia elimu sahihi ili kuhakikisha wanatoa ushirikiano unaohitajika,kwani serikali inatekeleza mradi huu kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi,Mhandisi Kepto Anosisye amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo una urefu wa kilomita 20.7 na unatekelezwa na kampuni ya kikandarasi toka China inayoitwa China Road and Bridge Corporation,kwa gharama ya shilingi bilioni 32.04.Ameongeza kuwa mkandarasi tayari ameanza kazi za awali ikiwemo uwasilishwaji wa mitambo,kuwasili kwa wafanyakazi mahususi wa mradi pamoja na usafishaji wa eneo la ujenzi.
Naye Mtendaji wa Kata ya Masoko,Bw. Martin Yuda Godwin,ameipongeza TANROADS kwa utoaji wa elimu kwa wananchi,akisema kuwa elimu hiyo imewajengea wananchi uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wao na maandalizi muhimu yanayohitajika kabla na wakati wa utekelezaji wa mradi.Ameongeza kuwa wananchi waliopata elimu hiyo watakuwa mabalozi wazuri wa kuwahamasisha wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki.
Kwa niaba ya wananchi,Bi. Emelia Razaro Mwainyekule mkazi wa Itandabala,ameishukuru serikali kwa utoaji wa elimu hiyo na kueleza kuwa ni miongoni mwa wananchi waliokuwa na makazi pamoja na makaburi ya ndugu zao ndani ya hifadhi ya barabara.Amepongeza utaratibu wa serikali wa kusimamia zoezi la uhamishaji wa makaburi kwa kuzingatia utu na sheria na kuahidi kutoa ushirikiano kwa kuondoa makazi yake katika hifadhi ya barabara ili kuwezesha utekelezaji wa mradi kwa mafanikio.