News

TANROADS YAHAKIKI UTHAMINI MRADI WA BARABARA YA KATUMBA–LUPASO, MBEYA

TANROADS YAHAKIKI UTHAMINI MRADI WA BARABARA YA KATUMBA–LUPASO, MBEYA

Mbeya.

28/01/2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umeendesha zoezi la uhakiki wa uthamini wa mali kwa wananchi walioguswa na Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Katumba–Lupaso yenye urefu wa kilomita 35.3 Mradi huo ni sehemu ya tatu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara ya Katumba–Mbambo–Tukuyu wenye jumla ya kilomita 79, unaotekelezwa mkoani Mbeya.

Zoezi la uhakiki linalenga kuthibitisha taarifa za uthamini kwa wananchi waliomo kwenye mpango wa fidia, ili kuhakikisha haki, uwazi na ushirikishwaji wa wananchi kabla ya utekelezaji wa mradi kuendelea.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, FRV Anna Deo Urassa, Mthamini Mwandamizi kutoka TANROADS, amesema kuwa katika baadhi ya maeneo usanifu wa barabara umeingia katika ardhi za wananchi, hivyo maeneo hayo yanastahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

Ameeleza kuwa uthamini wa awali ulifanywa na wathamini wa Serikali wa Mkoa wa Mbeya, huku hatua ya sasa ikihusisha uhakiki unaofanywa na wathamini wa TANROADS ili kujiridhisha na usahihi wa taarifa zilizokusanywa.

Uhakiki huo unahusisha kuthibitisha wananchi waliopo kwenye mpango wa fidia, mali zilizopo, hali na thamani ya mali hizo, pamoja na kubaini uwepo wa makaburi ili kuandaa mpango wa kuyahamisha endapo itahitajika.

Kwa mujibu wa FRV Urassa, maeneo mengi yanayopitiwa na mradi ni ardhi tupu, ambapo upimaji umefanyika kwa kutumia kifaa cha kisasa cha GNSS (RTK). Vipimo hivyo vitawekwa kwenye michoro ya usanifu wa barabara ili kuepusha dosari za kiufundi.Baada ya kukamilika kwa uhakiki, wathamini waliotekeleza uthamini wa awali watarudi kwa wananchi kuwaonyesha viwango vya fidia wanavyostahili kulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Uthamini Na. 7 ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018.

Kwa upande wake, PRV Saad Athuman amesema zoezi hilo ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka kati ya Serikali na wananchi, huku likisaidia kuzuia upotevu wa fedha za umma au malalamiko ya wananchi kupunjwa.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TANROADS Makao Makuu, Bi. Herieth Kamara, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusisitiza uhakiki wa uthamini, akisema zoezi hilo linapunguza migogoro na kuwezesha utekelezaji wa miradi kwa ufanisi.