News

WADAU WA BARABARA WAKUTANA: WAZIRI ULEGA AWEKA MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU YA SEKTA YA USAFIRISHAJI

WADAU WA BARABARA WAKUTANA: WAZIRI ULEGA AWEKA MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU YA SEKTA YA USAFIRISHAJI

Dar es salaam

28/01/2026

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, amezindua rasmi Kongamano la Wadau wa Sekta ya Barabara lililoandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (Tanzania Roads Association – TARA), lililofanyika katika Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kongamano hilo la kila mwaka huwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya barabara na miundombinu kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), taasisi za kitaaluma, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo. Miongoni mwa washiriki wa kimataifa ni wadau kutoka nchi za Kenya, Uganda, Namibia, Ghana na nyinginezo, ambapo mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa na wataalam na wadau wa sekta ya barabara kutoka Afrika.

Kongamano la mwaka huu limeongozwa na kaulimbiu isemayo: “Mageuzi ya Sekta ya Usafirishaji Barani Afrika yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi, kuimarisha muunganiko na kukuza uendelevu wa kiuchumi.”

Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Ulega alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa maono wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuwekeza kwenye upanuzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za mijini na vijijini, sambamba na kuimarisha vyanzo vya ufadhili wa matengenezo ya barabara nchini.

Aidha, Waziri Ulega alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha usalama barabarani, kudhibiti mizigo inayozidi uzito unaoruhusiwa, kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu, pamoja na kuzingatia masuala ya ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na uendelevu wa mazingira katika utekelezaji wa miradi ya barabara.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo hayo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wengine muhimu, wakiwemo vyama vya kitaaluma, taasisi za elimu ya juu, washirika wa maendeleo na sekta binafsi, ili kuhakikisha sekta ya barabara inakua kwa tija na uendelevu.

Akihitimisha hotuba yake, Mheshimiwa Ulega alisema kuwa mustakabali wa sekta ya usafirishaji barani Afrika unategemea mageuzi ya kina, uongozi imara na uwajibikaji wa pamoja. Aliongeza kuwa mikutano ya kila mwaka ya barabara ni jukwaa muhimu la kutafakari, kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuchukua hatua zitakazochangia kuongeza ufanisi, kuimarisha muunganiko na kukuza mifumo endelevu ya usafirishaji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.