KAMATI ZA KUSIKILIZA MALALAMIKO YA FIDIA KATIKA MRADI WA BARABARA YA MCHEPUKO UYOLE–SONGWE ZA ANZA KAZI RASMI JIJINI MBEYA
Mbeya.
27/01/2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha zoezi la kuunda Kamati za Kusikiliza na Kutatua Malalamiko yanayotokana na fidia kwa ngazi ya kata katika kata zote 12 zinazopitiwa na Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mchepuko ya Uyole–Songwe, jijini Mbeya. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha utekelezaji wa mradi unazingatia uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na haki kwa makundi yote yanayoguswa na mradi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mhandisi Msaidizi wa Mradi, Bw. Edwin Medard Kema, amesema kuwa kamati hizo zimeundwa mahsusi ili kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha malalamiko yao kwa uhuru kupitia wawakilishi wanaowafahamu na kuwaamini, badala ya kutoa malalamiko kwa njia zisizo rasmi. Ameeleza kuwa utaratibu huo utasaidia kupata suluhu za haki, za haraka na za kudumu kwa changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
Mhandisi Kema ameongeza kuwa kamati hizo zimeanza rasmi kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi, yakihusisha wote waliopo kwenye mpango wa fidia pamoja na wale ambao hawamo. Hii inalenga kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika kushiriki, kutoa changamoto zake na kupata majibu kwa wakati, jambo linaloimarisha uwazi, uwajibikaji na uaminifu kati ya wananchi na Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Shewa, Bw. Oscar Mwamaso, ameipongeza TANROADS kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuunda kamati hizo, akieleza kuwa zitakuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi, wakiwemo waliopo kwenye mpango wa fidia na wale wasiohusishwa moja kwa moja.
Naye Bw. Nahumu Kyando, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Shewa, Kata ya Mchangani, ameishukuru Serikali kwa kuwapa wananchi nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa kikamilifu katika mradi. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima iliyokuwa ikijitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa wanawake, Bi. Subira Wakson amesema kuwa wanawake wako tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo huduma za umama lishe na kazi za ujenzi kama kubeba zege. Amehimiza umuhimu wa kuzingatia na kuthamini mchango wa wanawake katika kata zote 12 zinazopitiwa na mradi.
Kwa ujumla, uundwaji wa Kamati za Kusikiliza na Kutatua Malalamiko unatarajiwa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi, kupunguza migogoro kati ya wananchi na mradi, kuwezesha upatikanaji wa majibu ya haraka kwa changamoto zinazojitokeza, na kuimarisha uaminifu kati ya wananchi na Serikali, hatua itakayochangia utekelezaji wa mradi kwa amani na maendeleo endelevu.