News

MAAFISA TEHAMA TANROADS WASHIRIKI KONGAMANO LA MAGEUZI YA KIDIJITALI

MAAFISA TEHAMA TANROADS WASHIRIKI KONGAMANO LA MAGEUZI YA KIDIJITALI

Dar es salaam

23/01/2026

Kitengo cha Maafisa TEHAMA kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kimeshiriki katika Kongamano la Tisa la Mwaka la TEHAMA lililofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Januari 2026 katika Ukumbi wa The Superdome, Masaki. Kongamano hilo lililenga kujadili masuala muhimu yatakayochochea maendeleo na mageuzi katika sekta ya TEHAMA nchini.

Kongamano hilo liliongozwa na kauli mbiu isemayo “Mageuzi ya kidigitali yanayochochea athari za kijamii na ubunifu wa kiteknolojia kwa taifa lenye ustawi, haki, ushirikishwaji na kujitegemea”, kauli mbiu inayosisitiza nafasi ya teknolojia katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.

Akizungumza kama mgeni rasmi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kifedha na kitaasisi ili kuchochea uvumbuzi wa kiteknolojia unaojenga ajira na kukuza kujitegemea kwa Taifa.

Aidha, Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa vijana katika mabadiliko ya kidijitali, akibainisha kuwa kupitia kampuni changa za TEHAMA (ICT Startups), vijana wana fursa kubwa ya kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa. “Ni azma ya Serikali kuhakikisha kundi hili linatambulika, linaendelezwa na linaungwa mkono ili kuboresha ubunifu wao,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA kutoka TANROADS, Bw. Haji Kabogo, alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau wa TEHAMA ili kujadili masuala mbalimbali ya kiteknolojia yatakayosaidia kuisogeza sekta hiyo kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Bw. Kabogo pia alimshukuru Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, kwa kutoa fursa kwa maafisa wa TANROADS kushiriki katika kongamano hilo, akieleza kuwa ushiriki huo umeongeza uzoefu, kubadilishana mawazo na wadau kutoka sekta nyingine, na kufungua fursa za kupata suluhisho bunifu zitakazosaidia kuboresha utendaji wa taasisi na sekta kwa ujumla.