News

SERIKALI YASHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA FIDIA NA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI KATA YA IJOMBE, MBEYA

SERIKALI YASHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA FIDIA NA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI KATA YA IJOMBE, MBEYA

Mbeya

23/01/2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea na zoezi la uundaji wa Kamati za Malalamiko ngazi ya Kata katika maeneo yanayopitiwa na mradi wa barabara ya mchepuo mkoani Mbeya, hatua inayolenga kushughulikia changamoto za fidia na kulinda maslahi ya wananchi wanaoathiriwa na utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza katika Kata ya Ijombe, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka TANROADS Makao Makuu, Herieth Kamara, amesema kuwa hadi sasa kata tano tayari zimetembelewa na zoezi hilo linaendelea katika kata nyingine. Ameeleza kuwa uundaji wa kamati hizo unaenda sambamba na utoaji wa elimu kuhusu uhifadhi wa barabara kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2009.

Kamara amesema wananchi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa kulinda barabara kwa matumizi ya sasa na ya baadaye, na wametakiwa kuwa mabalozi wa uhifadhi wa barabara kwa kutoa taarifa wanapobaini uvamizi au matumizi yasiyo sahihi katika maeneo ya hifadhi ya barabara. Amesisitiza kuwa matumizi ya maeneo tengefu ya barabara yanaruhusiwa tu kwa kupata vibali maalum kutoka ofisi za TANROADS.

Kwa upande wake, Mthamini Mwandamizi wa TANROADS, Anna Deo Urassa, amesema kuwa kabla ya kufikia hatua ya kuunda kamati za malalamiko, zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia lilifanyika kwa kuzingatia taratibu zote zilizopo. Amefafanua kuwa wananchi walipewa elimu, walishiriki katika zoezi la uthamini, walioneshwa viwango vya fidia na hatimaye kulipwa stahiki zao kabla ya kuanza kwa hatua nyingine za utekelezaji wa mradi.

Urassa ameongeza kuwa kamati za kusikiliza malalamiko ni utaratibu wa kawaida wa Serikali huundwa kwa mfumo shirikishi kuanzia ngazi za vijiji, ambapo wananchi, viongozi na wawakilishi wao hushiriki kwa uhuru ili kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa.

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo, Afisa Tarafa ya Tembela, Hodavia Webi, amesema kuwa barabara ya mchepuo itapunguza msongamano wa magari makubwa, hususan malori, katika barabara za Mbeya Mjini, hali itakayoboresha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na maendeleo ya wananchi wa maeneo ya vijijini.

Wananchi na viongozi wa Kata ya Ijombe wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo pamoja na ulipaji wa fidia kwa wakati. Wamesema elimu iliyotolewa imewawezesha kuelewa mipaka ya hifadhi ya barabara, taratibu za fidia na umuhimu wa kutoendelea kutumia maeneo yaliyolipwa fidia, wakisisitiza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa maendeleo ya Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.