News

WAKANDARASI WA MIRADI YA BRT WATAKIWA KUWEKA MPANGO MADHUBUTI WA KAZI ILI KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI

WAKANDARASI WA MIRADI YA BRT WATAKIWA KUWEKA MPANGO MADHUBUTI WA KAZI ILI KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI

Dar es salaam

22/01/2026

Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko, ametembelea na kukagua kwa siku mbili  utekelezaji wa miradi yote ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam, akiwataka wakandarasi kuongeza jitihada na kuimarisha mipango yao ya kazi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Nnko amesema ukaguzi huo ni wa endelevu na unalenga kufahamu kwa kina hatua za utekelezaji wa miradi, kubaini changamoto zilizopo na kutoa msukumo kwa wakandarasi kuongeza kasi na ufanisi wa utendaji wao.

Amebainisha kuwa kuchelewa kwa baadhi ya miradi kunatokana kwa kiasi kikubwa na wakandarasi kutokuwa na mipango madhubuti ya utekelezaji wa kazi, hali inayosababisha miradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Kwa ujumla, kuna miradi inayokumbwa na changamoto ya kuchelewa, hususan miradi ya BRT Awamu ya Nne (BRT 4) kuanzia katikati ya jiji kuelekea Mwenge, Ubungo na Tegeta. Miradi hii ipo nyuma ya ratiba, na changamoto kubwa imesababishwa na wakandarasi wenyewe kutokana na ukosefu wa mipango mizuri ya kazi.

 Hali hiyo imekuwa ni jambo la kuzingatiwa kwa uzito, na tayari TANROADS imechukua hatua za kusukuma utekelezaji pamoja na kuchukua hatua kali za kimkataba ili kuhakikisha kasi inaongezeka na miradi inakamilika kwa wakati, amesema Mhandisi Nnko.

Ameongeza kuwa kwa wakandarasi ambao hawajatekeleza miradi kwa viwango vinavyotarajiwa, hatua za kimkataba zikiwemo faini tayari zimeanza kuchukuliwa, huku akisisitiza kuwa hatua zaidi zitachukuliwa endapo ucheleweshaji utaendelea.

Pamoja na changamoto hizo, Mhandisi Nnko amepongeza maendeleo mazuri yanayoonekana katika baadhi ya miradi, ikiwemo mradi wa Ubungo – Kimara ambao umefikia takribani asilimia 70 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Aidha, amepongeza ujenzi wa Daraja la Jangwani ambao umefikia zaidi ya asilimia 30 na unaendelea vizuri ndani ya muda uliopangwa.

Amesisitiza wakandarasi kuendelea kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, hususan katika kipindi hiki ambacho hali ya hewa ni rafiki kwa utekelezaji wa miradi.

Mhandisi Nnko ametoa rai kwa wakandarasi na wahandisi wa TANROADS kufuatilia miradi kwa karibu ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora unaostahili, kwa gharama stahiki na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Vilevile, amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa changamoto za muda mfupi zitazaa manufaa ya muda mrefu pindi miradi itakapokamilika na kuanza kutoa huduma.