News

TANROADS YATEKELEZA UTARATIBU WA HAKI NA UWAZI KUPITIA KAMATI YA USULUHISHI WA MIGOGORO – MRADI WA UYOLE BYPASS

TANROADS YATEKELEZA UTARATIBU WA HAKI NA UWAZI KUPITIA KAMATI YA USULUHISHI WA MIGOGORO – MRADI WA UYOLE BYPASS

Mbeya

22/01/2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza rasmi zoezi la uundaji wa Kamati ya Usuluhishi wa Migogoro (GRC) kwa ajili ya Mradi wa Uyole Bypass (km 48.9) mkoani Mbeya. Barabara hiyo inatarajiwa kupita katika kata 12 na kugusa wananchi zaidi ya 2,638.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Solomon Itunda, amesema zoezi hilo linalenga kuhakikisha haki, uwazi na usawa vinazingatiwa kikamilifu katika mchakato mzima wa ulipaji wa fidia kabla, wakati na baada ya utekelezaji wa mradi.

 Ameeleza kuwa wataalamu wa TANROADS kutoka makao makuu pamoja na mkoa wa Mbeya wapo wilayani humo kwa ajili ya kusimamia uundwaji wa kamati za kata, hususan katika maeneo yaliyoathiriwa na mradi.

 Ameongeza kuwa Wilaya itaunda kamati ya ngazi ya Wilaya yenye jukumu la kusikiliza na kutatua malalamiko yote yatakayojitokeza wakati wa ulipaji wa fidia na utekelezaji wa mradi kwa ujumla.

Aidha, Mheshimiwa Itunda amewataka wananchi hususan waathirika wa mradi pamoja na viongozi wa kata husika kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maafisa wa TANROADS ili kuhakikisha mradi unatekelezwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza kwa niaba ya TANROADS, Afisa Msimamizi wa Hifadhi ya Barabara, Ndugu Christopher Chalange, amesema mikutano ya wananchi imefanyika kwa kuzingatia miongozo, taratibu na sheria zote za uthamini na ulipaji wa fidia. Amesisitiza kuwa katika Kata ya Inyala tayari kamati ya kushughulikia malalamiko ya fidia imeundwa, viongozi wake wamechaguliwa na wako tayari kupokea na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kwa wakati.

Kwa upande wake, Afisa Tarafa ya Isangati, Aron Sote, ameipongeza TANROADS kwa kupeleka timu ya wataalamu waliokutana na wananchi wa Kitongoji cha Mwashoma na maeneo mengine yaliyopitiwa na mradi. Amesema wananchi wamepatiwa elimu kuhusu taratibu za kuwasilisha malalamiko yao serikalini, huku kamati iliyoundwa ikitarajiwa kushughulikia changamoto za wananchi waliolipwa fidia pamoja na wale ambao bado hawajalipwa.

Naye Mtendaji wa Kata ya Inyala, Emmanuel Makau, amesema mkutano wa wananchi umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba ofisi ya kata itaendelea kupokea malalamiko ya wananchi kwa kipindi cha siku 14 kama ilivyokubaliwa. Amehimiza wananchi ambao hawakuhudhuria mkutano kufika ofisini ili kuwasilisha malalamiko yao kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Mmoja wa wanufaika wa fidia ya mradi huo, akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Wazo Talian, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na TANROADS Mkoa wa Mbeya kwa kulipa fidia kwa wakati.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iganjo, Eliud Mbogela, amesema ujenzi wa barabara ya mchepuo utapunguza kero za magari makubwa, kuongeza usalama barabarani na kuleta manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi, akieleza kuwa ana imani mradi utakamilika kwa wakati bila kuwaathiri wananchi.