News

UJENZI WA BARABARA YA KATUMBA–TUKUYU KWA KIWANGO CHA LAMI WAENDELEA, BILIONI 86 KUTUMIKA

UJENZI WA BARABARA YA KATUMBA–TUKUYU KWA KIWANGO CHA LAMI WAENDELEA, BILIONI 86 KUTUMIKA

Mbeya

22/01/2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kwa kasi kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Katumba – Tukuyu, ambapo utekelezaji umeanza rasmi katika sehemu ya tatu na ya nne za mradi huo zenye jumla ya gharama ya Shilingi bilioni 86. Hatua hii inalenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya pamoja na maeneo ya jirani.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo, Mhandisi Justine Mrope, amesema kuwa sehemu ya tatu ya mradi inaanzia Katumba hadi Lupaso yenye urefu wa kilomita 35.3, huku sehemu ya nne ikiwa na urefu wa kilomita 20.7. Ameeleza kuwa utekelezaji wa sehemu zote mbili unaendelea vizuri na kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa.

Mhandisi Mrope amefafanua kuwa sehemu ya tatu ya mradi inagharimu Shilingi bilioni 54, wakati sehemu ya nne ikigharimu Shilingi bilioni 32, fedha zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa viwango vya kisasa, ubora wa juu na kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, amesema Serikali tayari imekamilisha sehemu ya kwanza na ya pili ya barabara ya Katumba – Tukuyu kwa kiwango cha lami, na kwamba sehemu ya tatu na ya nne ndizo zilizobaki ambazo sasa zipo katika hatua ya utekelezaji.

 Sambamba na hilo, shughuli za ujenzi wa majengo ya kambi ya Mhandisi Mshauri nazo zinaendelea ili kuwezesha usimamizi mzuri wa mradi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mrope, utekelezaji wa sehemu ya tatu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36, huku sehemu ya nne ikitekelezwa kwa kipindi cha miezi 24. Ameongeza kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya China Roads & Bridge Co. Ltd (CRBC).

Amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo kwa kuwaunganisha kwa urahisi wakulima na masoko, hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa viazi, ndizi na parachichi.

Kwa upande wao, wananchi wa maeneo husika, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huo muhimu. Wamesema barabara ya Katumba hadi Busekelo itarahisisha usafirishaji wa mizigo, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza muda wa safari na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.