RTO NA TANROADS WAIMARISHA USHIRIKIANO WA USALAMA BARABARANI NA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU JIJINI MBEYA
Mbeya
21/01/2026
Kamanda wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Mbeya (RTO), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilena, leo Jumatano Januari 21, 2025, amekutana na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usalama barabarani mkoani humo.
Katika kikao hicho, SSP Kilena ameipongeza TANROADS kwa ushirikiano wanaouonyesha katika kuhakikisha barabara zinapitika na kutatua changamoto za miundombinu, hali inayochangia kupunguza msongamano wa magari, hususan katika barabara ya Mbalizi–Msalaga.
Aidha, ameishukuru TANROADS kwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika uwekaji na uboreshaji wa alama za barabarani, ikiwemo alama za kuongozea madereva, alama za tahadhari pamoja na vivuko vya watembea kwa miguu, hatua ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amemshukuru RTO kwa kikao hicho na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo.
Ameeleza kuwa TANROADS itaendelea kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya barabara, ikiwemo utanuzi wa barabara katika eneo la Mlima Nyoka pamoja na ujenzi wa mizunguko (roundabouts) katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari.
Hatua hizo zinalenga kuhakikisha barabara za Jiji la Mbeya zinapitika kwa misimu yote ya mwaka na kuongeza usalama kwa watumiaji wote wa barabara.