News

TANROADS YAANZA UPANUZI NA UJENZI WA BARABARA YA MCHEPUO MLIMA NYOKA KWENYE BARABARA YA TANZAM

TANROADS YAANZA UPANUZI NA UJENZI WA BARABARA YA MCHEPUO MLIMA NYOKA KWENYE BARABARA YA TANZAM

Mbeya.

20/01/2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza upanuzi na ujenzi wa barabara ya mchepuo katika eneo la Mlima Nyoka lililopo kwenye barabara ya TANZAM, kwa lengo la kupunguza ajali za mara kwa mara, msongamano wa magari na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hiyo muhimu kitaifa na kikanda.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa Barabara Kuu na Barabara za Mijini kutoka TANROADS, Mhandisi Nchama Wambura, amesema kuwa uamuzi wa kupanua barabara hiyo umetokana na ongezeko kubwa la magari, hususan malori makubwa, ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kupanda Mlima Nyoka na kusababisha ajali zinazoharibu mali na kupoteza maisha ya watu.

Mhandisi Wambura amesema Mlima Nyoka ni mrefu na mkali, hali inayosababisha magari mengi kukwama na kusababisha msongamano mkubwa wa magari, jambo lililoilazimu TANROADS kuanzisha ujenzi wa njia ya mchepuo pamoja na maeneo ya magari kupumzikia, ili kurahisisha mtiririko wa magari na kupunguza adha kwa madereva.

Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, TANROADS imezingatia masuala ya kijamii na kimazingira kwa kukutana na wananchi wa maeneo husika wakiwemo wazee wa mila na machifu, ili kujadili historia ya eneo hilo pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na ujenzi, ikiwemo uharibifu wa miti na chemchem za maji.

Kwa upande wake, Chifu Rocate Mwashinga ameipongeza Serikali kwa kuanzisha ujenzi wa barabara hiyo, akisema kuwa maendeleo ya wananchi hayawezi kupatikana bila miundombinu bora ya usafiri.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri kama sehemu ya kupanua wigo wa biashara wa ukanda wa SADC, ambapo barabara ya TANZAM ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa mizigo na abiria kutoka na kwenda nchi jirani.

Mhandisi Bishanga amesema kuwa changamoto za magari kukwama barabarani na katika milima zitapungua kwa kiasi kikubwa kufuatia utekelezaji wa mradi huo, unaogharamiwa na Serikali, na kutoa wito kwa wananchi na watumiaji wa barabara kufuata maelekezo yanayotolewa wakati wa ujenzi ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa kazi.