DARAJA LA SUNGWE LABORESHA USAFIRI KATIKA BARABARA YA TANZAM
Mbeya.
19/01/2026
Ujumbe wa wataalam kutoka TANROADS Makao Makuu kupitia Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi (TECU), kwa kushirikiana na TANROADS Mkoa wa Mbeya, umefanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Daraja la Sungwe lililopo katika barabara ya TANZAM mkoani Mbeya na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu pamoja na thamani ya fedha zilizotumika.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema daraja hilo limejengwa kufuatia madhara makubwa yaliyosababishwa na Kimbunga Hidaya pamoja na mvua kubwa za El Niño, ambazo zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika eneo hilo.
Ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa daraja jipya, eneo hilo lilikuwa na daraja la mita nne pekee ambalo lilikuwa dogo na kushindwa kupitisha maji wakati wa msimu wa mvua, hali iliyosababisha maji kufurika juu ya daraja na kuifanya barabara isipitike mara kwa mara, na hivyo kuleta changamoto kubwa kwa wasafiri, wasafirishaji na wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo.
Mhandisi Bishanga ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa barabara ya TANZAM kwa usafiri wa abiria na mizigo, Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya ujenzi wa daraja jipya lenye urefu wa mita 40, ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita moja pamoja na ufungaji wa taa za sola 40, hatua iliyoongeza usalama na uhakika wa usafiri katika vipindi vyote vya mwaka.
Aidha, amesema mradi huo umechangia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 200, huku wahandisi wazawa wakipata fursa ya kuongeza ujuzi na uzoefu wa kitaalamu, kwani ujenzi wake unasimamiwa na Kitengo cha Ushauri cha TANROADS (TECU), ambacho ni taasisi ya Serikali inayoendeshwa na wataalamu wazawa.
Ameeleza zaidi kuwa daraja hilo limejengwa kwa ubora unaotakiwa, akibainisha kuwa tabaka la juu la barabara limejengwa kwa safu tatu zenye uimara wa hali ya juu. Ameongeza kuwa barabara hiyo tayari imefunguliwa na imeanza kutumika, na kwamba ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mipango ya Serikali katika kutatua changamoto za muda mrefu katika barabara ya Tunduma–Igawa.
Kwa niaba ya wananchi, Freddy Julius Njinga kutoka Kijiji cha Songwe ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo, akisema kabla ya mradi huo walikuwa wakikumbwa na mafuriko makubwa yaliyowalazimu kuhama makazi yao kila msimu wa mvua. Ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kumehakikisha usalama wao na kuwaondolea hofu ya mafuriko, hivyo kuwawezesha kuishi kwa utulivu katika vipindi vyote vya mwaka.