MADARAJA MAPYA YA LUPA NA BITIMANYANGA KUFUNGUA FURSA ZA MAENDELEO KATI YA MBEYA NA SINGIDA
Mbeya
18/01/2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi (TECU) Makao Makuu, umepokea rasmi ujenzi wa madaraja mawili yaliyopo kwenye barabara ya Makongorosi–Rungwa, baada ya ukaguzi kubaini kuwa yamekidhi viwango vyote vya kihandisi na ubora.
Akizungumza wakati wa ukaguzi, Mhandisi Emmanuel Tang'ale, aliyemwakilisha Mhandisi Mkuu wa Kitengo Cha ushauri TANROADS (TECU) toka Makao Makuu, amesema ukaguzi ulilenga kuhakiki utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Lupa Tingatinga lenye urefu wa mita 46 pamoja na barabara zake za maingilio zenye urefu wa kilometa sita.
Amesema daraja hilo limekamilika, kufunguliwa na tayari linatumika, huku likiboresha usalama na upatikanaji wa huduma za usafiri kwa wananchi na watumiaji wa barabara hiyo.
Mhandisi Tang'ale ameeleza kuwa daraja la pili ni Daraja la Bitimanyanga, ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.3 na lina barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa tano, ambapo jumla ya gharama za madaraja hayo mawili ni shilingi bilioni 9.9.
Kwa mujibu wa TANROADS, madaraja hayo yamejengwa na mkandarasi mzawa Summer Communications Limited, na baada ya kukaguliwa kwa pamoja na timu za TANROADS Mkoa wa Mbeya na Makao Makuu, mkandarasi amekidhi masharti yote ya mkataba ikiwemo ubora wa ujenzi na uwekaji wa taa za barabarani.
Sambamba na hilo, amebainisha kuwa kukamilika kwa madaraja hayo kumeimarisha muunganiko wa barabara ya Makongorosi kuelekea Singida, akisisitiza kuwa barabara ya Makongorosi–Rungwa ni barabara ya kimkakati na ujenzi wa madaraja hayo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuiendeleza kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, mkandarasi, Mhandisi Isack Usaka amesema, utekelezaji wa miradi hiyo umefanyika kwa wakati na kwa ubora uliokubaliwa, umeongeza ajira kwa wananchi hususan vijana, na umeendelea kujenga imani ya serikali na wafadhili kwa wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu.