News

NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI ZANZIBAR AVUTIWA NA DAKTARI WA BARABARA

NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI ZANZIBAR AVUTIWA NA DAKTARI WA BARABARA

Zanzibar, 15 Januari, 2026

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Zanzibar, Mhe. Badria Atai Masoud amevutiwa na maelezo yanayohusu mtambo maalum wa kukagua barabara, mara baada ya kukamilika kujengwa unaofahamika zaidi kama Daktari wa Barabara (Roads Doctor).

Mhe Badria, alipotembelea banda la maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara la Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) yanayoendelea kufanyika Dimani-Fumba Zanzibar, kwa ajili ya kupata maelezo mbalimbali, yanayohusiana na ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Baada ya kupata maelezo mbalimbali kutoka kwa taalamu Mhe. Badria alionesha nia ya kufahamu zaidi kuhusu kazi za mtambo huo aliosema ni muhimu kuwepo Visiwani pia, ili kupima ubora wa barabara zinazoendelea kujengwa kwa usimamizi wa wizara yake na kupitia Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS).

Mhe. Badria pia alielezewa matumizi ya hifadhi ya barabara ambazo ni fursa kwa kuingizia serikali fedha kutokana na malipo ya walioomba na kupewa mkataba kulingana na shughuli watakazofanya kwenye hifadhi hiyo.

“Sisi kama Wizara tunashirikiana na ZANROADS katika shughuli za ujenzi, lakini pia nimefahamishwa kuna mashirikiano baina yao na nyie TANROADS, hivyo tunahitaji kufahamu zaidi taratibu muhimu za kabla, wakati na baada ya ujenzi, ikiwemo hili gari ambalo mnasema ni mtambo wa kupima viwango na ubora wa barabara kabla ya kuanza kutumika,” amesema Mhe. Badria.

Awali akitoa maelezo kuhusu mtambo wa kupima ubora wa barabara, Mhandisi Miradi wa TANROADS, Cecilia Kalangi amesema mtambo huo unasaidia kupima ubora wa barabara kwa kutumia vifaa maalumu vilivyofungwa kwenye mtambo husika.

Naye Meneja Mazingira na Jamii wa TANROADS, Bi. Zafarani Madayi amesema sheria za hifadhi ya barabara zinatekelezwa tangu mwaka 1932 na zimeendelea kuboreshwa na sasa zilizofanyiwa marekebisho kidogo za mwaka 2025, zinazoruhusu watumiaji wa hifadhi hizo kuhakikisha wanaomba kibali na kupewa mkataba wa miaka mitano na kuendelea na shughuli zao, na baadae endapo TANROADS itahitaji eneo lake kwa ajili ya kuliendeleza wahusika wanapewa taarifa na kuondoa, ili kupisha ujenzi.