News

TANROADS YAKAGUA MIRADI YA DHARURA YA CERC MKOANI MBEYA

TANROADS YAKAGUA MIRADI YA DHARURA YA CERC MKOANI MBEYA

Mbeya.

16/01/2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Kitengo chake cha Usimamizi wa Miradi (TECU) imefanya ukaguzi wa miradi ya dharura inayotekelezwa kupitia utaratibu wa Contingency Emergency Response Component (CERC), huku wananchi wakionyesha kuridhika na utekelezaji wa miradi hiyo.

Ujumbe wa wataalamu kutoka Makao Makuu ya TANROADS, ukiongozwa na Mhandisi Tang’are,aliemuwakilisha Mhandisi Mkuu wa kitengo Cha ushauri Cha TANROADS (TECU) Lutengano Mwandambo,  ulifika mkoani Mbeya kukagua miradi hiyo na kuthibitisha kuwa kazi zote zimekamilika kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu.

Akizungumza mbele ya ujumbe huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, alisema ukaguzi huo ni muhimu katika kuthibitisha ubora wa miradi na kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya dharura mkoani humo.

Ukaguzi wa kwanza ulifanyika Januari 13, 2026, katika Daraja la Sungwa lililopo kwenye Barabara ya TANZAM, barabara ya kimkakati inayounganisha Tanzania na nchi jirani. Daraja hilo, lililojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.5, awali lilikuwa halipitiki wakati wa mvua, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara.

Kukamilika kwa daraja hilo sasa kumeongeza usalama na kurahisisha usafiri, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hiyo muhimu.