TANROADS YATOA MAFUNZO YA AWALI KWA WATUMISHI WAPYA WA UMMA
Dar es salaam
15/01/2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) imeanza kutoa mafunzo ya awali elekezi kwa watumishi wapya wa Serikali waliopata ajira kupitia mfumo wa Ajira Portal. Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Januari, 2026, yakiwa na lengo la kuwaandaa watumishi hao kuanza utumishi wa umma kwa misingi ya maadili, weledi na uwajibikaji.
Mafunzo hayo yameongozwa na Meneja wa Rasilimali Watu wa TANROADS, Bw. Pilika Kasanda, akiwa ameambatana na maafisa wengine wakiwemo Bi. Felister Banda, Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi kutoka TANROADS Makao Makuu, Bw. Severin Lukinga, Afisa Rasilimali Watu Daraja la Kwanza, pamoja na Bw. Ausi Nchimbi, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Bw. Kasanda alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaandaa watumishi wapya kwenda kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kwa maslahi mapana ya wananchi, hususan katika maeneo yenye changamoto kama vile vituo vya mizani ya magari.
“Tumesikia mara kwa mara malalamiko yanayohusisha vituo vya mizani. Tunatarajia nguvu kazi hii mpya itakwenda kusaidia kumaliza changamoto hizo. Ajira hizi si fursa ya kujitajirisha binafsi, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi,” alisema Kasanda.
Aidha, aliwataka watumishi wapya kubadilisha mitazamo, mienendo na tabia walizokuwa nazo kabla ya kujiunga na utumishi wa umma, na kuwa vielelezo bora katika jamii wanazoihudumia kwa kuzingatia maadili na misingi ya kazi za Serikali.
Kasanda alisisitiza kuwa watumishi wote wa umma hufanya kazi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mujibu wa Ibara ya 35 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Dhamana uliyopewa kama mtumishi wa umma ni kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake kwa wananchi. Hivyo, ni lazima kila mtumishi atimize wajibu wake kwa uaminifu, nidhamu na uadilifu wa hali ya juu,” aliongeza.
Pia aligusia suala la rushwa, akibainisha kuwa limeendelea kuwa changamoto kubwa katika utumishi wa umma, hususan katika sekta ya mizani ya magari. Aliwataka watumishi wapya kupinga na kupambana dhidi ya vitendo vya rushwa, akieleza kuwa kupitia mafunzo hayo, TANROADS inalenga kujenga mfumo wa utendaji usio na mianya ya rushwa.
Kwa upande wake, Bw. Ausi Nchimbi, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea watumishi wapya uelewa wa kina kuhusu maana ya utumishi wa umma, majukumu yao, pamoja na namna Serikali inavyotekeleza majukumu yake kwa wananchi.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi mpya kupatiwa mafunzo ya awali elekezi kabla ya kuanza kazi rasmi ili kuwajengea misingi imara ya utendaji.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wapya, Bw. Martine William, Afisa Mizani Daraja la Pili wa TANROADS, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu TANROADS na majukumu yake.
“Tunashukuru kwa fursa hii ya mafunzo. Tangu siku ya kwanza tumepata mwanga mkubwa, hasa kuhusu historia ya TANROADS, majukumu yake na namna inavyotekeleza kazi zake,” alisema Martine.
Naye Bi. Janeth Martine Jonas, mmoja wa watumishi wapya, aliishukuru TANROADS kwa kuwapatia mafunzo hayo, akisema yamewajenga kitaaluma na kuwapatia ujasiri katika utekelezaji wa majukumu yao pindi watakapoanza kazi rasmi katika maeneo yao ya kazi.