News

TANROADS KAGERA YAKAGUA MIRADI YA DHARURA INAYOTEKELEZWA NA WAKANDARASI WAZAWA

TANROADS KAGERA YAKAGUA MIRADI YA DHARURA INAYOTEKELEZWA NA WAKANDARASI WAZAWA

Kagera

14, January 2026

Watumishi wa TANROADS mkoani Kagera, wakiongozwa na Meneja wa Mkoa, Mhandisi Samwel Joel Mwambungu, wamefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya dharura ya ujenzi wa madaraja matano ya Kanoni, Kyetema, Kyanyabasa, Kalebe na Kamishango. Miradi hiyo inatekelezwa katika wilaya za Bukoba, Bukoba Vijijini na Muleba na wakandarasi wazawa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 45.6.

Ziara hiyo imelenga kujionea kwa karibu namna Serikali, kupitia TANROADS, inavyotekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa kuwashirikisha na kuwaamini wakandarasi wazawa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Mwambungu, amesema kuwa miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari mwaka huu. Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kagera, ikiwemo kurahisisha usafiri, biashara na shughuli za kijamii.

Aidha, Meneja huyo amewashukuru wananchi kwa uvumilivu wao wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na amewasihi kuitunza na kuilinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

Mhandisi Mwambungu pia ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na Wizara ya Ujenzi kwa usimamizi mzuri unaohakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.

Kwa niaba ya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo, mwakilishi wa kampuni ya Milembe Construction, Mhandisi Oscar Byabato, ameishukuru Serikali kwa kuwaamini wakandarasi wazawa na kuwapatia fursa ya kutekeleza miradi hiyo. Amehakikisha kuwa wakandarasi wataendelea kutekeleza miradi hiyo kwa ubora unaotakiwa na ndani ya muda uliopangwa ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Kwa nyakati tofauti, watumishi wa TANROADS Mkoa wa Kagera wameeleza kufurahishwa na kupata fursa ya kutembelea na kukagua miradi hiyo adhimu inayotekelezwa katika wilaya za Muleba, Bukoba na Bukoba Vijijini, wakisisitiza dhamira ya Serikali ya kuboresha miundombinu kwa maendeleo ya wananchi.