News

MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA MSALATO WAFIKIA HATUA YA UKAMILISHAJI, WAZIRI MBARAWA APONGEZA USIMAMIZI WA PAMOJA

MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA MSALATO WAFIKIA HATUA YA UKAMILISHAJI, WAZIRI MBARAWA APONGEZA USIMAMIZI WA PAMOJA

Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaoendelea jijini Dodoma umefikia hatua ya ukamilishaji (finishing), huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti na ushirikiano wa taasisi zote zinazohusika ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.

Akizungumza Januari 14, 2026 jijini Dodoma wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, amesema hatua ya mwisho ya ujenzi inahitaji umakini mkubwa, matumizi sahihi ya fedha na uhakika wa ubora wa vifaa vinavyowekwa ili kuendana na mahitaji ya uwanja wa ndege wa kimataifa.

Mheshimiwa Profesa Mbarawa amezipongeza taasisi zote zinazoshiriki katika usimamizi wa mradi huo, ikiwemo Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kwa kushirikiana vyema katika kuhakikisha ujenzi unaendelea kwa mpangilio na kwa weledi.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu baina ya TANROADS, TAA, TCAA pamoja na idara za zimamoto na uhamiaji ni muhimu ili mifumo na vifaa vya uendeshaji wa uwanja huo visomane na kurahisisha utoaji wa huduma mara baada ya uwanja kufunguliwa rasmi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, amesema Wakala umejipanga kusimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa. Ameongeza kuwa TANROADS imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na tayari imeanza kuyafanyia kazi.

Naye Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, Bw. Clemence Mbaruk, amesema uongozi wa uwanja huo umejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa viwango vyote vinavyotakiwa, huku watumishi 170 tayari wakiwa wameshahamishwa kwenda Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi mara baada ya uwanja kufunguliwa rasmi.

Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 370, na unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, kwa kuruhusu ndege za aina mbalimbali za kitaifa na kimataifa kutua na kutoa huduma katika uwanja huo.

Aidha, Mheshimiwa Profesa Mbarawa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Africa Growing Together Fund.