News

"TUNZENI BARABARA ZIDUMU KWA MUDA MREFU" - MHANDISI KASEKENYA

“TUNZENI BARABARA ZIDUMU KWA MUDA MREFU” - MHANDISI KASEKENYA Arusha, 10 Januari, 2026 Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa viongozi mkoani Arusha kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kutunza na kulinda miundombinu inayojengwa ili idumu kwa muda mrefu, kupendezesha na kuchochea ukuaji wa mji huo wa utalii nchini. Akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mianzini - Olemringaringa-Sambasha hadi Ngaramtoni Km 18 Mhandisi Kasekenya amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza msongamano, ajali na mafuriko jijini Arusha na hivyo kukuza hadhi ya jiji hilo. "Arusha ni mji wa utalii unaopokea wageni wengi hivyo Serikali waelimisheni wananchi ili wafahamu kuwa barabara, madaraja na taa ni za wananchi hivyo wazitunze na kuondoa dhana kuwa miradi ya maendeleo ni ya Serikali", amesema Mhandisi Kasekenya. Amewataka wananchi na madereva kuheshimu alama za barabarani na kuacha tabia ya kuvamia hifadhi ya barabara kufanya biashara au ufugaji kwani kufanya hivyo kunasababisha msongamano, ajali, uharibifu wa barabara na mafuriko wakati wa mvua. "Zaidi ya Shilingi Bilioni 23 zinatumika kujenga barabara hii ili kulifungua jiji la Arusha, kupunguza msongamano na kulipendezesha, ili kuwa jiji la mfano na kuvutia wageni na matukio mbalimbali nchini", amesisitiza Naibu Waziri huyo wa Ujenzi. Amemtaka mkandarasi STECOL COOPERATION anaejenga mradi huo kuhakikisha unakamilika ifikapo Julai 2026. Katika hatua nyingine Mhandisi Kasekenya amekagua ujenzi wa daraja la Tanganyeti lenye urefu wa mita 40 katika barabara kuu ya Arusha - Namanga na kuelezea kuridhishwa na kasi ya mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 95. Nae Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi na Mbunge wa Arumeru Magharibi Jones Lukumay wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara na madaraja mkoani humo na kuahidi kuisimamia miradi hiyo ili ilete tija kwa wananchi. Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe amemhakikishia Naibu Waziri kuwa miradi yote inayotekelezwa mkoani humo inatoa fursa kwa vijana na wanawake wenyeji kupata ajira na ujuzi ili kuiendeleza miradi hiyo inapokamilika. Amesema daraja la Tanganyeti litakamilika Januari 15, 2026 na kumaliza kero katika eneo hili.