News

MIRADI YA DHARURA KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI NYASA NA SONGEA VIJIJINI.

MIRADI YA DHARURA KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI NYASA NA SONGEA VIJIJINI.

9/12/2025

Ruvuma

Mhandisi Mkuu wa Kitengo cha Ushauri cha Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS–TECU), Lutengano Mwandambo, amefanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kukagua utekelezaji wa miradi ya dharura ya ujenzi wa Madaraja ya Mkili na Mitomoni, inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Miradi hiyo inatekelezwa kufuatia uharibifu wa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mvua kubwa za El Niño na Kimbunga Hidaya, hali iliyosababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara katika maeneo husika na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Mwandambo amesema kwa ujumla utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri, huku akiwahimiza wakandarasi kuendelea kuzingatia masharti ya mikataba, hususan muda wa utekelezaji, ubora wa kazi na masuala ya usalama.

Ameeleza kuwa ziara hiyo imefanyika wakati huu kutokana na kuanza kwa msimu wa mvua, ikiwa ni sehemu ya jitihada za TANROADS kuhakikisha miradi ya dharura inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kwamba hatua zote za kiufundi na kiusalama zinafuatwa kikamilifu, licha ya uwepo wa wasimamizi wa kila siku kwenye maeneo ya miradi.

Mhandisi Mwandambo ameongeza kuwa Madaraja ya Mkili na Mitomoni yapo kwenye barabara muhimu zinazotumika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo ya jirani, akibainisha kuwa kukatika kwa barabara hizo hapo awali kuliathiri kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa watu na mazao pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii, hali iliyodhoofisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi kutoka TANROADS Makao Makuu, Emmanuel Tang’ale, amesema jumla ya miradi miwili ya dharura ya Madaraja ya Mkili na Mitomoni inagharimu Shilingi bilioni 12.39.

Amesema Mradi wa Daraja la Mkili unagharimu Shilingi bilioni 3.19 na unatekelezwa na mkandarasi mzawa, BR Associate Construction, ambapo unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 20 pamoja na kazi za barabara za kuingilia darajani zenye urefu wa mita 200 upande mmoja na  800 upande mwingine.

Ameongeza kuwa Mradi wa Daraja la Mitomoni unagharimu Shilingi bilioni 9.2 na unatekelezwa na mkandarasi Ovans Construction, ambapo unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 45, ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita 8.8 pamoja na ujenzi wa makalvati (box culverts) 12, huku miradi hiyo ikiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji na ikitarajiwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Naye Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Ferdinand Mdoe, amesema miradi hiyo ya dharura ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji na kwamba wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhandisi Mkuu wa Kitengo cha Ushauri kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya miradi pamoja na watumiaji wa barabara hizo kuzingatia alama za usalama barabarani na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi, ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa usalama, ufanisi na bila kuathiri shughuli za kila siku za wananchi.