News

TANROADS YATOA ELIMU KATIKA MAONESHO YA ZITF

TANROADS YATOA ELIMU KATIKA MAONESHO YA ZITF

Zanzibar, 07 Januari 2026Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kupitia Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar (ZITF) yanayoendelea katika viwanja vya Fumba Dimani, Zanzibar.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mhandisi Perpetua Kisamba kutoka TANROADS amesema kuwa wakala huo unatoa elimu mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kutunza hifadhi ya barabara, udhibiti na upimaji wa uzito wa magari yanayobeba mizigo pamoja na masuala ya utunzaji wa mazingira.

Ameeleza kuwa elimu hiyo inatolewa kwa wageni wote wanaotembelea banda la TANROADS bila kujali wanatoka Zanzibar au Tanzania Bara.“Elimu hizi tunazotoa ni kwa kila mgeni anayefika katika banda letu, wakiwemo wakazi wa Zanzibar pamoja na wageni waliotoka Bara,” amesema Mhandisi Kisamba.

Aidha, amesema kwa sasa TANROADS inasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 37,435.04, zikiwemo barabara kuu na za mikoa, ambapo baadhi zimejengwa kwa kiwango cha lami na nyingine kwa kiwango cha changarawe.

Ameongeza kuwa kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inayolenga kujenga na kukuza ukuaji wa biashara inaendana kikamilifu na majukumu ya TANROADS, kwani wakala huo huhakikisha barabara zinapitika wakati wote ili kuwezesha mazao ya wakulima kufika sokoni kwa wakati, bidhaa kuwafikia walaji kwa urahisi, pamoja na kufungua fursa zaidi za biashara kwa wafanyabiashara kufika maeneo mbalimbali nchini.

Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar yalianza rasmi tarehe 29 Desemba, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Januari, 2026.