MADARAJA YA KYANYABASA, KALEBE, KYETEMA, KAMISHANGO NA KANONI KUWA MKOMBOZI WA USAFIRI MKOA WA KAGERA
Kagera, 31 Desemba 2025
Madaraja ya Kyanyabasa (mita 105), Kalebe (mita 60), Kyetema (mita 45), Kamishango (mita 45) na Kanoni (mita 30) yanayoendelea kujengwa mkoani Kagera yakikamilika yataimarisha usafiri salama na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwa wakazi na watumiaji wa barabara hizo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo inayotekelezwa chini ya utaratibu wa Miradi ya Dharura (CERC), Meneja wa Udhibiti wa Mikataba kutoka Kurugenzi ya Ununuzi na Mikataba TANROADS, Mhandisi Musa Madirisha Kaswahili, amesema miradi hiyo itawezesha wananchi kusafirisha mazao ya biashara kwa uhakika na kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Kagera una jumla ya miradi mitano (5) ya CERC inayotekelezwa katika maeneo ambayo awali yalikuwa korofi, hususan wakati wa mvua za masika. Mhandisi Kaswahili ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo muhimu.
Amesema madaraja hayo yatawanufaisha watumiaji wa barabara kuu ya Mutukula – Bukoba – Kalebezo, pamoja na kuimarisha mawasiliano na mikoa ya Geita, Shinyanga na Kigoma, sambamba na nchi jirani ya Uganda.
Aidha, ameeleza kuwa miradi hiyo inaunganisha mtandao wa barabara za mkoa na bandari ya Bukoba, ambayo ni lango kuu la usafiri wa majini katika Ziwa Victoria, hususan kupitia daraja la Kanoni.
Kwa mujibu wake, awali wananchi walikuwa na hofu ya kuvuka hasa wakati wa mvua kutokana na kujaa kwa maji, lakini ujenzi wa madaraja haya mapya na ya kisasa utaondoa changamoto ya mafuriko na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Julius Ryoba Festo, amesema daraja la Kyanyabasa lenye urefu wa mita 105 na upana wa mita 11.3 limefikia asilimia 70 ya ujenzi, daraja la Kalebe (mita 60, upana mita 11.1) asilimia 70, na daraja la Kyetema (mita 45, upana mita 11.3) limefikia asilimia 75.
Ameongeza kuwa daraja la Kamishango (mita 45, upana mita 11.1) limekamilika kwa asilimia 97, huku daraja la Kanoni (mita 30, upana mita 18.9 lenye njia nne) likiwa limefikia asilimia 77. Madaraja yote hayo yanatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa wa usafiri na uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Mhandisi Festo amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na umaliziaji wa matuta ya barabara unganishi katika madaraja ya Kyanyabasa, Kalebe na Kyetema, huku mihimili ya chuma kutoka nje ya nchi ikitarajiwa kuwasili muda wowote kwa ajili ya umaliziaji wa deck slab.
Kwa madaraja ya Kamishango na Kanoni, ujenzi wa kingo na kuta za kuzuia mmomonyoko unaendelea, pamoja na maandalizi ya ufungaji wa taa za barabarani. Kwa mujibu wa mpango kazi uliopo, madaraja yote matano yanatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 20 Januari 2026.
Naye Msimamizi wa Miradi kutoka Kitengo cha Wahandisi Washauri cha TANROADS (TECU) – Kagera, Mhandisi Christian N. Mbise, amesema kwa sasa changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ni mvua nyingi zinazoathiri ratiba za kazi na kusababisha ugumu wa kazi.
Mhandisi Mbise ameongeza kuwa miradi yote mitano ya CERC inatekelezwa na wakandarasi wazawa; Kampuni ya Gemen Engineering ikijenga madaraja ya Kyanyabasa na Kyetema, Milembe Construction daraja la Kalebe, D.R.K General Merchants daraja la Kamishango, na Abemulo Company daraja la Kanoni.
Wakati wa ziara ya ukaguzi, Mhandisi Musa Kaswahili amewataka wakandarasi na wasimamizi wa miradi kujipanga kufanya kazi kwa zamu za mchana na usiku ili kufidia muda uliopotea na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Abdallah Mfinanga, Mtaalamu wa Ununuzi na Ugavi kutoka TANROADS Makao Makuu, amesisitiza wakandarasi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia ubora wa hali ya juu, akieleza kuwa Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 zimeweka kipaumbele kwa wakandarasi na washauri wazawa kushiriki katika miradi mikubwa ya kitaifa.