News

KASEKENYA AIPA TANROADS SIKU10 KUJA NA MPANGO KAZI UJENZI WA BARABARA NA MADARAJA ILEJE

KASEKENYA AIPA TANROADS SIKU10 KUJA NA MPANGO KAZI UJENZI WA BARABARA NA MADARAJA ILEJE

24/12/2025

Mbeya

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuja na mpango kazi unaotekelezeka utakaowezesha ujenzi wa barabara na madaraja wilayani Ileje kukamilika kwa wakati.

Amesema hayo leo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Isongole-Isoko km 52 na madaraja ya Sange na Kalewesi ambayo ujenzi wake unaendelea wilayani humo.

" Natoa siku 10 wataalam na wakandarasi wanaojenga miradi hii mje na ufumbuzi wa namna gani miradi hii itakamilika kwa wakati bila kuathiri huduma za usafiri na uchukuzi", amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amesema Serikali inataka miradi ikamilike kwa wakati kwasababu fedha zipo na kusisitiza kuwa kuanzia sasa msimamizi atakaeshindwa kumsimamia mkandarasi kuendana na mpangokazi atahesabiwa kuwa hatoshi.

Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Songwe Eng. Frederick Mande amesema wakala huo umejipanga kuhakikisha barabara  mkoani humo zinapitika wakati wote hususan kipindi hiki cha mvua bila kuathiri huduma za uchukuzi na usafiri.

Nae mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi  ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa miundombinu Wilayani humo ambayo imechangia fursa za ajira kwa vijana na wanawake na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wakandarasi ili miradi hiyo ilete tija na ufanisi kwa ustawi wa wananchi.