News

SH BILIONI 14.5 ZABADILISHA MAISHA: DARAJA LA NZALI LAANZA KUTUMIKA DODOMA.

SH BILIONI 14.5 ZABADILISHA MAISHA: DARAJA LA NZALI LAANZA KUTUMIKA DODOMA.

22 Disemba 2025

Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameleta tabasamu kwa wananchi wa Nzali na Itiso baada ya kuanza kutumika kwa Daraja la Nzali lililogharimu Sh bilioni 14.5. Alisema daraja hilo ni suluhisho la changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwa miaka mingi, hususan wakati wa mvua.

Akizungumza katika hafla ya kuruhusu matumizi ya daraja hilo, Senyamule alisema kabla ya ujenzi wake wananchi walikumbwa na adha mbalimbali ikiwemo vifo vya watu na mifugo, kupotea kwa mali, wagonjwa kushindwa kufika hospitalini kwa wakati, watoto kukosa masomo na wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao.

Alisema Rais Samia, kwa kujali maisha na ustawi wa wananchi, aliamua kupeleka fedha hizo Nzali ili kuhakikisha wananchi wanapata daraja litakalowawezesha kufanya biashara, kupata huduma za afya kwa wakati na watoto kuhudhuria shule bila vikwazo. Aliongeza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 98 na daraja limeanza kutumika rasmi huku kazi ndogondogo zikiendelea.

Senyamule aliwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa daraja hilo kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kusafirisha mazao na kuendeleza biashara, sambamba na kuwa walinzi wa miundombinu hiyo, akisisitiza kuwa Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaoharibu au kuiba miundombinu hiyo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Janeth Mayanja, alisema daraja hilo ndo lilikuwa ajenda yake ya kudumu kwa  Mbunge wa Chamwino Mh. Deo Ndejembi kwa sasa anadhani ajenda hii inaisha baada ya Daraja hili kukamilika hili lilikuwa ni mpango wake na maono yake na aliweza kulisemea vizuri nankuliwasilisha kwenye mamlaka zinazohusikana hatimaye serikali ikatoa fedha na kazi kama tunavyoona Leo

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alisema ujenzi wa daraja hilo ulianza Novemba 15, 2024 na unahusisha daraja lenye urefu wa mita 60 na upana wa mita 11.4, makaravati manne pamoja na barabara ya maingilio yenye urefu wa kilomita 1.5, huku Daraja hili likifikia asilimia 98 huku asilimia mbili zilizobaki zikitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 30 mwaka huu.