News

ULEGA AMWELEKEZA MKANDARASI BARABARA YA AMANI MAKORO - RUANDA

ULEGA AMWELEKEZA MKANDARASI BARABARA YA AMANI MAKORO - RUANDA

 Ruvuma, 22 Desemba, 2025

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi kuweka kipaumbele cha utu na kuondoa kero kwa wananchi kila wanapopewa kazi za ujenzi hapa nchini kwani huo ndio mwelekeo wa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mkoani Ruvuma, Ulega amesema kila kwenye kazi ya ujenzi, ni muhimu kwa mkandarasi kuweka mazingira rafiki kwa watumiaji wa eneo linalofanyiwa ujenzi, ili kurahisisha maisha ya wakazi na kulinda utu wao badala ya kufikiria kumaliza ujenzi wa barabara. 

“Kama umepewa kazi ya ujenzi, fikiria unawezaje kurahisisha maisha ya watu? Kama unaweza kuweka kalvati kuzuia maji yasiingie kwenye nyumba za watu, weka kwanza kalvati halafu endelea na ujenzi.,” amesema Ulega.

Ulega ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kitahi - Amani Makoro - Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi (Km 85) kwa kiwango cha lami unaotekelezwa na kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG).

Waziri Ulega amefanya ziara hiyo baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye alionesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ingawa serikali tayari imemlipa mkandarasi huyo.

 Akiwa katika eneo la mradi, Ulega alimtaka mkandarasi huyo kuongeza bidii katika ujenzi wa barabara hiyo, ili kuwaondolea kero wananchi, ambapo Serikali haipendi kuona wananchi wakiteseka kwa mambo, ambayo yanaweza kumalizwa.

Waziri Ulega amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anajenga vivuko vya watembea kwa miguu, kuongeza upana wa mitaro na urefu wa makalavati katika eneo la Amani Makoro sambamba na ufungaji wa taa za barabarani kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro, ili kurahisisha shughuli za biashara kuendelea hadi nyakati za usiku.

Yapo maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan atakapomaliza kazi anataka kuona wananchi wake wawe na nyuso za furaha na tabasamu hivyo basi hakikisheni ujenzi wa barabara na madaraja unazingatia utu wa wananchi, ili tutatue changamoto na kuleta tabasamu”, amesema Waziri Ulega

Waziri Ulega pia amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS)  Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha anatengeneza maegesho ya malori katika hifadhi ya barabara eneo la Amani Makoro, ili magari hayo yasisimame pembezoni mwa barabara na kuharibu miundombinu hiyo.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Mkwama ameeleza kuwa mradi wa barabara hiyo umegawanyika katika sehemu tatu na unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 60.4. 

 Mhandisi Mkwama, amesema kuwa sehemu ya kwanza ya Km 5 kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro imekamilika na sasa Mkandarasi anaendelea na sehemu ya pili ya kuanzia Amani Makoro hadi Ruanda Km 35, ambayo imefikia asilimia 41 ya utekelezaji wake.

Ameeleza kuwa sehemu hiyo ya pili ilipaswa kukamilika mwezi Desemba 2025 lakini imeshindakana kutokana na changamoto mbalimbali ambazo baadhi tayari Serikali imeshazichukuliza hatua na zingine zinaendelea kuchukuliwa za mara kwa mara ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo mwezi Aprili, 2026.

Mhandisi Mkwama amemuahidi Waziri Ulega kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa ikiwemo ya ufungaji wa taa za barabarani, ambazo kwenye mradi huo zipo 880 kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi

Akitoa maelezo yake, Afisa Mwajiri kutoka kampuni ya CRSG, Bw.  Themistocles Rugabela, ameiomba radhi serikali kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana kwa ubora, ili kukamilisha ujenzi huo.

Awali, wananchi wa eneo la Amani Makoro walimuomba Waziri Ulega kutatua kero ya vivuko vya watembea kwa miguu katika barabara hiyo, ambapo kwa sasa ni kero kwa wanafunzi na wakazi wengine kuvuka kwenye mitaro iliyojengwa maana hakuna sehemu ya kuvukia.