News

BODI YA USHAURI YA TANROADS YARIDHISHWA NA UJENZI WA DARAJA LA PANGANI

BODI YA USHAURI YA TANROADS YARIDHISHWA NA UJENZI WA DARAJA LA PANGANI

Tanga, 21 Desemba, 2025

Bodi ya Ushauri (MAB) ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani, unatekelezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ‘scaffolding system installation’ inayoongeza ufanisi na ubora wa ujenzi wa madaraja makubwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya bodi hiyo kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa MAB, Mhandisi Amin Mcharo, amesema wamefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi pamoja na matumizi ya teknolojia ya hali ya juu katika kusogeza na kujenga daraja hilo ya ‘scaffolding’, ambayo ni mfano wa ubunifu unaopaswa kuigwa katika miradi mingine ya barabara na madaraja inayotekelezwa nchini.

Amesisitiza kuwa bodi inatarajia mradi huo utakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

“Tumeshuhudia kazi ikiendelea vizuri kwa kutumia teknolojia mpya ya scaffolding, bodi imeridhishwa na hatua zilizofikiwa na tunatarajia mradi huu utakamilika kwa wakati,” alisema Mhandisi Mcharo.

Ameendelea kwa kusema kuwa, bodi inatamani miradi yote ya TANROADS  itekelezwe kwa kasi na ubora unaoonekana katika mradi wa Daraja la Pangani.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwahusisha wataalam wa ndani ili kujenga uwezo wao kitaalamu kupitia kujifunza teknolojia mpya zinazotumika katika miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 525 umefikia asilimia 70, ambapo linajengwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu inayolenga kuhakikisha uimara na usalama wa miundombinu hiyo kwa muda mrefu.

Mhandisi Besta amesema kuwa daraja hilo litakapokamilika litaunganisha miji ya Bagamoyo na Dar es Salaam kwa upande mmoja, na kuunganisha mkoa wa Tanga na mpaka wa Horohoro kuelekea Mombasa kwa upande mwingine.

Halikadhalika, amebainisha kuwa daraja hilo ni sehemu ya mradi wa barabara unaotekelezwa chini ya Mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaounganisha Bagamoyo na Lungalunga.