Uharibifu wa mazingira ni chanzo cha mafuriko - Mhandisi Massawe
Arusha, 19 Desemba, 2025
Ofisi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Arusha imeeleza baadhi ya wakazi wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakifanya uharibifu wa mazingira kwa kujenga kuta za matofali kwenye mkondo wa maji, ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha mafuriko pindi mvua inaponyesha.
Akifanya ukaguzi akiwa na timu yake ya matengenezo pamoja na Mhandisi Nchama Wambura kutoka Makao Makuu ya TANROADS, Meneja wa
TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe amesema wamelazimika kufanya ukaguzi huo baada ya kuona maji mengi yakipita
pembezoni mwa barabara ya Bypass ya Arusha iliyojengwa mwaka 2018 kwenda Namanga, na pia mikoa ya Dar es Salaam na Tanga na baadaye
kuingia kwenye makazi ya wananchi, na wamebaini kuwa nyumba nyingi zimejengwa kiholela bila kuzingatia ramani za mipango miji kumesababisha kuzuia mkondo wa maji.
Mhandisi Massawe amesema yeye na timu yaye alioongozana nayo wamegundua pia ujenzi wa misingi, kuta za matofali ziliyojengwa pamoja na mitaro iliyojengwa kwa mawe, ambayo yote imesababisha maji kushindwa kupita kwenye njia yake na kusababisha kusambaa kwenye makazi ya majirani zao ambao hawajajenga ukuta.
“Kutokana na ujenzi holela bila kuzingatia mipango, pia bila kuangalia aina za udongo, maana ardhi ya hapa ni volkano udongo wake ni mwepesi na ni rahisi kusombwa na maji ya mvua na kusababisha makorongo makubwa kutokana na kasi ya maji kuwa kubwa pia,” amesema Mhandisi Massawe.
Hatahivyo, Mhandisi Massawe amewashauri wakazi wa maeneo mbalimbali ya Arusha wakiwemo wa Ngaramtoni - Kibaoni kuzingatia mabadiliko ya tabianchi yanayojitokeza, ambapo sasa jijini la Arusha limekuwa na maji mengi takribani miaka miwili sasa.
“Niwaombe wananchi na viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha viwanja vinapimwa kabla ya ujenzi ili waweze kuacha mikondo ya maji, ili yaweze kuelekea kwenye mito
Naye Mkazi wa Ngaramtoni mtaa wa Kibaoni, Bi. Anna Edward amesema ameishi eneo hilo takribani miaka mingi, na sasa anawatoto wanne na wajukuu, ambapo awali maji ya mvua yalikuwa yakisambaa kila mahali, na hata baada ya ujenzi wa barabara kuu yalitengenezewa njia na kupita vizuri.
“Shida imeanza miaka miwili iliyopita kutokana na kuta zilizojengwa maji yakakosa mwelekeo na sasa yamekuwa yakisambaa kila mahali na kusababisha mafuriko kwenye nyumba yangu, naiomba sana serikali ituangalie maana nyumba yangu inasombwa na maji haya ni mengi sana,” ameomba Bi. Anna.
Kwa upande wake Bw. Nathan Malisa naye mkazi wa eneo hilo, ameomba maji hayo yaelekezwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara kwa kujengwa mtaro mkubwa.