TANROADS NA TECU MSIMAMIENI MKANDARASI - MHANDISI KASEKENYA
Mbeya, 20 Desemba, 2025
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amemwelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoani Mbeya kushirikiana na Mhandisi Mshauri TECU kumsimamia mkandaradi CRBC anaejenga barabara za Mbaka-Kibanja Km 20.7 na Katumba-Lupaso Km 35.3, ili zikamilike kwa wakati.
Naibu Waziri amesema hayo leo tarehe 20 Desemba, 2025 alipokagua ujenzi wa barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu Km 79.4 wilayani Rungwe.
"Hakikisheni ujenzi unaendelea kwa viwango na barabara haijifungi wakati wote wa ujenzi, ili shughuli za usafiri na uchukuzi zisiathirike", amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Amesisitiza ujenzi wa barabara zote mbili za Mbaka-Kibanja Km 20.7 na Katumba- Lupaso Km 35.3 uende sambamba, ili ukamilike kwa pamoja na kuleta tija kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Sulemani Bishanga amesema tayari ujenzi wa barabara hizo umeanza na umefikia asilimia 4.6 na utatekelezwa ndani ya miezi 36.
Naye Mbunge wa Busokelo, Mhe. Lutengano Mwalwiba ameishukuru Serikali kwa kasi ya ujenzi wa barabara hizo, ambazo zimetoa ajira na kukuza ujuzi kwa vijana wa Rungwe.
Halikadhalika, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jafari Haniu amemshuku Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo na kumhakikishia mkandarasi ushirikiano wakati wote na kusisitiza kukamilika kwa barabara hizo kutachochea ukuaji wa biashara ya mazao ya biashara na chakula na hivyo kukuza uchumi wa wananchi wa Rungwe na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla.
Ujenzi wa barabara ya Mbaka-Kibanja Km 20.7 na Katumba- Lupaso Km 35.3 ni mkakati wa Serikali kuifungua Wilaya ya Rungwe kwa barabara za lami, ambapo tayari sehemu ya Lupaso-Bujesi Km.10, Bujesi-Mbaka Km 12.6 na Kibanja-Tukuyu Km 7 ujenzi wake umekamilika.