News

WAZIRI MKUU Dkt. MWIGULU AAGIZA UJENZI WA BARABARA NJIA NNE TUNDUMA

WAZIRI MKUU Dkt. MWIGULU AAGIZA UJENZI WA BARABARA NJIA NNE TUNDUMA

Songwe, 18 Desemba, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameagiza ujenzi wa barabara njia nne eneo la Tunduma ili kupunguza msongamano.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miundombinu mkoani Songwe,  Dkt. Mwigulu amezitaka taasisi zote za Serikali kushirikiana, ili ujenzi huo uanze mara moja na hivyo kuufanya mpaka wa Tanzania na Zambia katika eneo la lango kuu la SADC kufanya kazi kwa tija na hivyo kuvutia wasafirishaji na wasafiri wengi.

" Miundombinu ikiwa bora huduma zikiimarishwa, amani na nidhami vikiwepo uchumi wa watu na taifa kwa ujumla utaimarika", amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema tayari Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), umeanza maandalizi ya upanuzi huo katika eneo lenye urefu wa mita 700 kuwa njia nne.

Naibu Waziri Mhandisi Kasekenya amesema mkakati mwingine wa kupunguza msongamano ni kujenga mzani eneo la Iboya ili kupima magari yanayotokea mjini Tunduma na kuipunguzia msongamano mzani ya Mpemba, ambayo itapima magari yatokayo Mbeya kwenda Tunduma.

Naibu Waziri Kasekenya amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa changamoto zilizojitokeza katika mzani ya Mpemba zimerekebishwa na sasa unafanyakazi kwa ufanisi.