News

TANROADS YAFAFANUA KITAALAM KUHUSU BARABARA YA DODOMA-GAIRO 

TANROADS YAFAFANUA KITAALAM KUHUSU BARABARA YA DODOMA-GAIRO

Dodoma, 15 Desemba, 2025 

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma wametoa ufafanuzi wa kitaalam kuhusu barabara ya Dodoma - Gairo kutokana na taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha kipande cha barabara kilichojengwa chini ya kiwango katika eneo la makaravati Wilayani Kongwa.

 Akitoa ufafanuzi huo, Mhandisi Mkazi wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Elisony Mweladzi, amesema kipande hicho chenye urefu wa mita 300 kilijengwa mahususi kwa ajili ya majaribio kabla ya kuwekwa tabaka la mwisho la lami hatua ambayo ni ya kawaida katika miradi ya ujenzi wa barabara.

“Kwa kawaida kabla ya kuweka lami, huwa unaweka eneo la majaribio kwa hiyo Mkandarasi anapewa eneo ya mita 300 kwa ajili ya majaribio kuona kama vipimo vyote vya lami vinakidhi viwango”, amesema Mhandisi Elisony. 

Amesema baada ya kipande hicho kupimwa na maabara ya TANROADS, ilibainika kuwa hakikukidhi viwango vilivyokubaliwa, jambo lililosababisha Mamlaka hiyo kumwandikia barua Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuanza mara moja kufanya marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza ikiwemo kukiondoa kwa gharama zake. 

Mhandisi Elisony amesisitiza  kuwa TANROADS itaendelea kumsimamia kwa karibu Mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi unazingatia viwango na thamani ya fedha za umma.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka kwa Mkandarasi Kings Builders anayetekeleza ujenzi wa mradi huo, Edward Njau amekiri kupokea barua kutoka TANROADS kwa ajili ya kufanya marekebisho, na ameahidi kutekeleza maelekezo hayo mara moja.