News

TANROADS ARUSHA YAWATAKA WANANCHI WANAOVAMIA HIFADHI ZA BARABARA KUFUATA SHERIA

TANROADS ARUSHA YAWATAKA WANANCHI WANAOVAMIA HIFADHI ZA BARABARA KUFUATA SHERIA

Arusha, 04 Desemba, 2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Arusha imewaonya wananchi wanaovamia hifadhi za barabara na kufanya shughuli zisizoruhusiwa, ikiwemo biashara na ujenzi usiofuata taratibu, kwa kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Akizungumza jijini Arusha, Mhandisi Christopher Saul kutoka TANROADS Arusha amesema hifadhi za barabara zipo kisheria na matumizi yake yameainishwa wazi, hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia sheria na kanuni za barabara ili kuepuka usumbufu na madhara yasiyo ya lazima.

“Wananchi wote wanaohitaji kutumia maeneo ya hifadhi ya barabara wanapaswa kuwasiliana na ofisi za TANROADS ili kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuanza shughuli zozote. Hii itasaidia kuepusha migogoro na uharibifu wa miundombinu,” alisema Mhandisi Saul.

Kwa mujibu wa TANROADS, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiendesha shughuli kama maosheo ya magari (Car Wash), gereji, welding, pamoja na biashara ndogondogo za machinga na mama lishe katika maeneo ya hifadhi za barabara, jambo linalosababisha adha kwa watumiaji wa barabara hasa watembea kwa miguu.

Imeelezwa kuwa katika baadhi ya maeneo ya jiji la Arusha, njia zilizotengwa kwa watembea kwa miguu zimegeuzwa kuwa maegesho ya magari madogo na makubwa, hali inayowalazimisha watembea kwa miguu kutumia barabara kuu na kuhatarisha usalama wao.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na vyombo vya habari wamekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na wameomba mamlaka husika kuhakikisha watembea kwa miguu wanaachwa kutumia maeneo yao yaliyotengwa ili kupunguza ajali za mara kwa mara.

Aidha, TANROADS imewakumbusha wananchi kuhakikisha maeneo ya hifadhi za barabara yanabaki wazi wakati wote ili kuepuka ajali na uharibifu wa miundombinu. 

Imeelezwa kuwa maji yanayotoka kwenye maosheo ya magari na shughuli za upishi, gereji, au kilimo pembezoni mwa barabara yamekuwa yakisababisha uharibifu wa barabara.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Saul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara zenye ubora, zinazozingatia watembea kwa miguu na mifumo bora ya maji.