“MENEJA WA TANROADS ARUSHA NI KIJANA HODARI NA MCHAPAKAZI ANAFANYA KAZI VIZURI” - RC MAKALLA
Arusha, 30 Novemba, 2025
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amepongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, kutokana na kasi na ubora wa usimamizi wa miradi ya ujenzi mkoani humo.Mhe. Makalla ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa imeridhishwa na utendaji kazi wa Mhandisi Massawe, hususan katika kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa na Wizara ya Ujenzi.
RC ameeleza kuwa imani yake ni kwamba Meneja huyo ataendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na ufanisi katika kuhakikisha maelekezo yote ya Waziri wa Ujenzi yanatekelezwa kwa wakati.
Naye Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassar naye ameungana na RC Makalla na kusema Mhandisi Massawe amekuwa msikivu na anatenda kwa wakati kazi za ujenzi mbalimbali ambazo zimepita kwenye jimbo lake.
“Sina shida kabisa na Meneja Massawe tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na kumshauri kutokana na huku ni jimbo nililodumu kwa vipindi tofauti na awali nilikuwa mkuu wa wilaya pia nalijua vizuri,” amesema Mhe. Nassar.Aidha, Mhandisi Massawe amepewa majukumu kadhaa ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu muhimu ndani ya Mkoa wa Arusha, na ameonyesha utayari pamoja na uwezo wa kuyakamilisha kwa kiwango bora kinachotarajiwa na Serikali.Kwa pamoja, viongozi hao wametoa kauli inayodhihirisha ushirikiano mzuri kati ya Mkoa na TANROADS katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia miundombinu madhubuti na salama.