News

SERIKALI KUONGEZA TAA ZA BARABARANI ENEO LA KING’ORI JIJINI ARUSHA

SERIKALI KUONGEZA TAA ZA BARABARANI ENEO LA KING’ORI JIJINI ARUSHA

 Arusha, 30 Novemba, 2025

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) itaongeza taa 20 za barabarani eneo la King’ori Jijini Arusha.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amegiza sehemu zote za barabara zinazostahili kusimikwa taa, ili kusaidia shughuli mbalimbali ziendelee na zitapunguza uhalifu kutokana na kuwa na mwanga na halikadhalika zitapendezesha mandhari ya eneo husika.

Mhe. Ulega amepongeza kwa kasi ya ujenzi unaoendelea ambapo anauhakika utakamilika kwa wakati, ambapo pia ameagiza apelekewe mpango wa barabara ya Tengeru-Mbuguni, ambayo itarahisisha na kupunguza foleni.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe amesema katika mradi wa ujenzi wa dharura wa barabara ya eneo la King’ori - KIA JCT - Namanga utasimikwa taa za barabarani 85 na baadaye utaongezwa 20 katika eneo la Malula.

Mhandisi Massawe amesema ujenzi wa barabara hiyo umehusisha ujenzi wa maboksi kalavati makubwa matatu, barabara ya mchepuko yenye urefu wa Km1.5; uinuaji wa tuta mita 672; kujenga barabara ya chini Km 1, kujenga tabaka la juu Km 1 na usimikaji wa taa 85.

Amesema ujenzi huo unaofanywa na kampuni ya wazawa ya M/s Abemulo Contractors Co Limited ya kutoka Bukoba, hadi sasa umefikia asilimia 94 za utekelezaji, ambapo sasa wanasubiri kuwasili kwa lami, ili iwekwe na kukamilisha ujenzi, ambapo mkataba unatakiwa kukamilika tarehe 15 Desemba, 2025, hadi sasa wapo ndani ya muda.

Mhandisi Massawe amesema kuwa kwa mkoa wa Arusha unamiradi mingine ya ujenzi wa daraja la mita 40 eneo la Namanga na daraja jingine limejengwa katika barabara ya Arusha-Minjingu eneo la Kisongo.

Awali Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassar alimuomba Mhe. Ulega kuongezwe taa katika kipande cha eneo la Malula, ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea kwa binadamu na mifugo inayovushwa kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine, ambapo awali hakikuwekwa taa hizo.

Halikadhalika, Mhe. Nassar ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa boksi kalavati pamoja na kunyanyua tuta la barabara hiyo, ambapo wakazi wake na watumiaji wengine walikuwa wakisumbuka na mafuriko ya mara kwa mara kila mvua zinaponyesha.