WAKAZI WA LINDI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA MIRADI YA DHARURA
Lindi, 27 Novemba 2025
Wakazi wa mkoa wa Lindi, hususan wa Somanga–Mtama, wameishukuru Serikali kupitia TANROADS kwa kuondoa kero ya mafuriko kupitia ujenzi wa madaraja na makalavati makubwa.
Mzee Kimbwembwe, maarufu eneo hilo, aliyasema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliyekagua miradi inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango wa dharura wa CERC. Amesema Serikali imekuwa bega kwa bega na wananchi kuhakikisha usalama wao kupitia ujenzi wa daraja la Somanga, ambalo lilikuwa halipitiki wakati wa mafuriko.
Amepongeza juhudi za viongozi wa mkoa, wilaya ya Kilwa, na wahandisi wa TANROADS kusimamia ujenzi wa awali na unaoendelea, hatua iliyowezesha kunyanyua tuta la barabara na kujenga daraja kubwa litakalomaliza kabisa tatizo la mafuriko kama ya miaka 2023 na 2024 wakati wa mvua za El-Nino.
Ameeleza kuwa uchumi wa Kusini umefunguka kutokana na uchimbaji wa makaa ya mawe unaohitaji barabara imara, hivyo ujenzi huo utarahisisha usafirishaji wa mizigo. Aidha, amesema miundombinu bora itakuza biashara kwa wakazi wa Lindi.
Bi. Hadija Kamlambe kutoka Somanga amesema wamepata nafuu kubwa kwani barabara na madaraja yalikuwa yakikatika kipindi cha mvua, lakini sasa wanauhakika wa kwenda mashambani bila tatizo. Bi. Zuhura Abdallah amepongeza na kumtakia kheri Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ujenzi huo muhimu unaounganisha Dar es Salaam na mikoa ya Kusini. Naye Bi. Fatuma Hassan amewashukuru wajenzi wa madaraja kwa kazi kubwa itakayowaondolea changamoto za usafiri wakati wa mvua.
Waziri Ulega ameridhishwa na kasi ya ujenzi, ambapo daraja la Somanga–Mtama (mita 60) limefikia asilimia 89, daraja la Mikereng’ende (mita 40) asilimia 90.6, na daraja la Matandu (mita 60) asilimia 86.7; yote yanatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Desemba 24, 2025.
Kutokana na athari za mafuriko, Serikali imeidhinisha utekelezaji wa miradi 13 mkoani Lindi: Barabara kuu ya Marendego–Mingoyo (miradi 5), Barabara ya Tingi–Kipatimu (mradi 1), Nangurukulu–Liwale (miradi 3), Liwale–Nachingwea (miradi 2), na Kiranjeranje–Namichiga (miradi 2). Miradi hiyo inatekelezwa na kampuni saba, zikiwemo nne za wazawa na tatu za kimataifa, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri TECU, Mkoa wa Lindi.