News

“Miradi ya Madaraja ya Dharura Lindi Yafanikishwa 100% — Waziri Ulega Apongeza”

“Miradi ya Madaraja ya Dharura Lindi Yafanikishwa 100% — Waziri Ulega Apongeza”

Lindi

26 Novemba, 2025

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amehitimisha ziara yake ya siku mbili katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Lindi, iliyoangazia ukaguzi wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Akiwa katika mradi wa ujenzi wa madaraja ya dharura katika eneo la Somanga–Mtama, amesema kwa ujumla Serikali inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, huku akiwataka wataalamu kuongeza nguvu zaidi katika usimamizi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Mhe. Waziri Ulega, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emily Zengo, alieleza kuwa utekelezaji wa miradi 13 ya dharura, ikijumuisha madaraja 11 pamoja na makaravati 18, unaogharimu shilingi bilioni 119.1. Miradi hiyo ni matokeo ya athari za mvua za El-Nino zilizonyesha kati ya Desemba 2023 na Machi 2024, ambazo zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na hivyo kukatisha mawasiliano kati ya mikoa ya kusini na maeneo mengine nchini.

Aidha, Mhandisi Zengo aliongeza kuwa mradi huo unatekelezwa na jumla ya kampuni 7, zikiwemo kampuni 4 zinazomilikiwa na wakandarasi wazawa na kampuni 3 zinazomilikiwa na wageni. Alisema kuwa mpaka kufikia sasa, utekelezaji wa miradi hiyo umefikia asilimia 88.

Akizungumza na wananchi katika mradi wa daraja la Somanga–Mtama lenye urefu wa mita 60, linalojengwa na kampuni ya Hunan Construction Engineering Ltd ya China, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliipongeza kampuni hiyo kwa usimamizi mzuri unaoendana na ubora wa viwango na kusisitiza kuwa Serikali inafarijika kufanya kazi na kampuni za aina hiyo.

“Kwa ujumla mimi binafsi nimeridhika na hatua iliyofikiwa. Sasa naomba nichukue fursa hii kuwapongezeni nyote wana Lindi kwa kazi nzuri iliyofanyika. Ni dhahiri kuwa bila nyinyi na wataalamu wenu kuwa mstari wa mbele, ingewawia vigumu kampuni ya Hunan Construction Engineering Ltd kufanikisha mradi huu. Hongereni sana,” alisema Waziri Ulega.

“Naomba niwahakikishie, ninapotoka hapa ninampelekea Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan salamu za matumaini. Nitamweleza kuwa zile bilioni 119 alizowaletea kutekeleza miradi hii hakukosea. Salamu nyingine nitamwambia kuwa ndani ya fedha hizo, wakandarasi wazawa zaidi ya nusu ya wakandarasi wote wamepata fursa ya kushiriki kwenye mradi, na pia vijana wazawa na wananchi wengi nao wamefaidika kwa ajira,” alisisitiza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo, ameishukuru Serikali kwa kuujali Mkoa wa Lindi, na kusema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati kutasaidia kuharakisha maendeleo ya wakazi wa Lindi na maeneo jirani.