PWANI FUNGUENI BARABARA YA ZAMANI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI KATIKA BARABARA KUU YA MOROGORO – DAR ES SALAAM: WAZIRI ULEGA
Pwani
26 Novemba, 2025
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemwagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani kuandaa utaratibu wa kuifungua barabara ya zamani iliyokuwa ikitumika kupitisha magari Kutoka Dar es Salaam – Morogoro kwenda mikoa mingine sehemu inayoanzia picha ya ndege hadi mlandizi kama njia ya kukabiliana na tatizo la foleni.
Waziri Ulega ametoa agizo hilo akiwa akatika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara katika mikao Dar es Salaam, Pwani na Lindi ambapo amewaagiza Mameneja wa TANROADS katika Mikoa yote nchini kuandaa mpango kazi wa dharula utakaosaidi kupunguza kero ya foleni katika barabara zinazopitisha magari mengi.
Akitolea mfano matumizi ya kipande cha barabara kuu ya Morogoro kati ya Picha ya Ndege Kibaha na Mlandizi ambacho ni sehemu ya barabara ya zamani iliyokuwa ikitumika kabla ya ujenzi wa mradi wa barabara mpya inayotumika hivi sasa, Waziri Ulega amesema endapo kipande hicho kitafufuliwa na kuanza kutumika kitakuwa mwarobaini wa tatizo la foleni katika barabara hiyo.
“Nichukue fursa hii kutoa maelekezo hususani kwa wenzetu Mkoa wa Pwani, fanyeni kila muwezalo hakikisheni mnaifungua barabara ya zamani, msisubiri mpaka mvua zianze tatizo litakuwa pale pale, jengeni utaratibu wa kuwa na suluhisho kabla ya tatizo ninaamini mkifanya hivyo mtakuwa mfano wa maeneo mengine” alisisitiza Mhe Ulega.
Katika ziara hiyo pia Mhe Waziri Ulega alipata fursa ya kukagua na kujionea mradi wa ujenzi wa Makalavati ya zege katika sehemu ya pili eneo la tuta la daraja la Mkapa mradi unaofadhiliwa na benki ya dunia kwa gharama ya shilingi bilioni 12.4 ambapo amemwagiza mkandarasi kampuni ya M/S Kings Builders Limited kkukamilisha kazi hiyo kabla ya muda ili waweze kuelekeza nguvu katika maeneo mengine ya mradi.
“Ndugu wataalamu nimejionea mwenyewe namna mnavyopambana kuhakikisha tunafikia malengo, naomba niwasisitize ongezeni kasi tukamilishe kazi hii mapema, mvua ziko njiani, mkimaliza hapa hamisheni mitambo katika eneo jingine lenye uhitaji zaidi muendelee kuchapa kazi” aliongeza Waziri Ulega.
Kuhusu maelekezo ya serikali ya kuzipa kipaumbele kampuni za Wazawa, Mhe Ulega amesema serikali imejiwekea mkakati wa kuzipa kazi Kampuni zinazomilikiwa na wazawa ilimradi ziwe na sifa halikadhalika historia yake ionyeshe weledi na ufanisi katika miradi iliyowahi kutekelezwa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Babueli Shija amemhakikishia Waziri Ulega kuwa wataalamu wanaendelea kusimamia kwa karibu mradi huo ambao mpaka sasa umefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake na kwamba wanatarajia ifikapo Disemba 27, 2025 kazi hiyo itakuwa imekemilika.