News

TANROADS DAR ES SALAAM JIWEKEENI MKAKATI WA KUPUNGUZA FOLENI ZINAZOCHELEWESHA SHUGHULI ZA MAENDELEO: MHE. ABDALLAH ULEGA, WAZIRI WA UJENZI

TANROADS DAR ES SALAAM JIWEKEENI MKAKATI WA KUPUNGUZA FOLENI ZINAZOCHELEWESHA SHUGHULI ZA MAENDELEO: MHE. ABDALLAH ULEGA, WAZIRI WA UJENZI

Dar es Salaam

26 Novemba, 2025

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amewaagiza Mameneja wa TANROADS nchini kuhakikisha wanatengeneza mpango kazi madhubuti wa kukabiliana na changamoto ya foleni, jambo ambalo amesema linachangia kuzorotesha shughuli za uchumi.

Waziri Ulega ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika eneo la Kongowe, mkoani Dar es Salaam, kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 3.8 kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 54.5. Amesema kuwa Serikali haiko tayari kuwaona wananchi wake wakishindwa kutekeleza shughuli za maendeleo kutokana na tatizo la foleni.

“Ndugu zangu wakazi wa Kongowe, Serikali yenu kwa kutambua umuhimu wa eneo hili na changamoto kubwa ya msongamano wa magari, imeamua kuwekeza mabilioni ya fedha kujenga barabara ambayo sasa magari yatakuwa yakipita bila bugudha. Bila shaka kila mmoja wenu amejionea jinsi kazi zinaendelea,” alisema Waziri Ulega.

“Kama haitoshi, Mhe. Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa heshima ya Wanakongowe pia ametuletea fedha za kujenga daraja la juu yaani (flyover) ili kuhakikisha magari yanapita kwa urahisi na wakati huo huo wananchi wanaendelea na shughuli zao bila kukwazika,” alisisitiza Mhe. Ulega.

Aidha, Waziri Ulega pia alitumia fursa hiyo kumuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Lazeck Kyamba, kuhakikisha anaweka bango maalum litakaloonyesha taarifa za mradi huo wa ujenzi wa daraja ili wananchi waweze kuuelewa.

Akijibu maombi ya wakazi wa Kongowe yaliyowasilishwa kwake na Ndugu Adam Said Mkere kwa niaba ya wananchi wenzake kuhusu umuhimu wa kutengeneza barabara ya Vicheji pamoja na ile ya kutoka Mwembetegu hadi Vikindu Polisi, Mhe. Ulega amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inatambua changamoto hiyo na tayari imeweka bajeti ya kuzijenga barabara hizo.

Halikadhalika, Waziri Ulega amemwagiza mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya M/s Stecol Corporation, ambaye hadi sasa amelipwa kiasi cha shilingi bilioni 8.1, kufanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Lazeck Kyamba, amemuhakikishia Waziri Ulega kuwa timu ya wataalamu iko makini kusimamia mradi huo kila hatua. Ameongeza kuwa maagizo yote aliyoyatoa, ikiwemo kuhakikisha wazawa wanapewa kipaumbele cha ajira katika mradi huo, yanatekelezwa ipasavyo.